27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

DPP akusanya bilioni 3.6, nyumba 11 zataifishwa

NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

SERIKALI kupitia Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), imeingiza zaidi ya Sh bilioni 3.6 na kutaifisha nyumba sita za washtakiwa waliokuwa wakikabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ndani ya wiki moja.

Hayo yamebainika kutoka na idadi ya watuhumiwa waliokiri makosa Oktoba 4 na Oktoba 7 mpaka 11 mwaka huu katika mahakama hiyo.

Oktoba 4, mshtakiwa Yasin Katera aliyekuwa akishtakiwa pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi Takukuru, Godfrey Gugai alilipa faini ya Sh milioni 100 na Serikali ikataifisha nyumba yake moja iliyopo Nyegezi Mwanza.

Alilipa faini hiyo baada ya kukiri kosa la kutakatisha fedha huku akijua fedha hizo ni zao la kuficha ukweli baada ya kudai ni mmiliki wa nyumba wakati nyumba ni mali ya rafiki yake, Gugai.

Mfanyabiashara Magdalena Uhwello na Halima Nsubuga walikiri makosa ya kutakatisha fedha wakahukumiwa kulipa  faini ya Sh milioni 101 na fedha zao  Dola za Marekani 388,000 kutaifishwa na Serikali.

Mahakama iliamuru washtakiwa wakishindwa kulipa  fedha hizo wataenda jela mwaka mmoja kwa kosa la kuendesha upatu na wataenda jela  miaka 20 kwa kutakatisha fedha.

Oktoba 7-11 wafanyabiashara watatu,  Mohammed Yusufali, Arifali Paliwalla na Sameer Khan walilipa fidia Sh 1,201,000,000 baada ya kukiri makosa yao na nyumba nne zilizopo Bagamoyo na Masaki zilitaifishwa na kuwa mali ya Serikali.

Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Elinaza Luvanda. DPP aliwapunguzia mashtaka kutoka  544 na kubakia mashtaka matatu.

Akisoma Mashtaka hayo, Wakili wa Serikali Mkuu Oswald Tibabyekomya alidai, shtaka la kwanza na la pili linamkabili Mshtakiwa Yusufali pekee.

Kwamba katika vipindi tofauti kati ya Januari 2008 hadi Januari 2016 jijini Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Farm Plant Limited, kwa nia ya kukwepa kodi aliwasilisha retuns (marejesho) za kugushi kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kusababisha ukwepaji wa kodi wa zaidi ya Sh bilioni 21.

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa kati ya Agosti mwaka 2015 hadi Januari mwaka 2016, kwa vitendo kama hivyo, mshtakiwa huyo alisababisha ukwepaji wa kodi wa Sh 1,684,559,546.47.

Shtaka la tatu la washtakiwa wote ambapo ilidaiwa kuwa kati ya Januari 2008 hadi Januari mwaka 2016 kwa vitendo vyao vya uwasilishwaji wa nyaraka za uongo za ulipaji kodi, waliisababishia TRA hasara ya Sh 24,303,777,426.70.

Mahakama iliamuru mshtakiwa Yusufali alipe fidia ya hasara aliyoisababishia TRA ya zaidi ya Sh bilioni 24 na tayari alishalipa sh bilioni moja.

Alidai, kiasi kilichobaki kitalipwa kwa muda wa miezi 24 ambapo kila mwezi atalipa sh 970, 990,726.08 pamoja na kutaifishwa kwa nyuma nne zilizo maeneo ya Masaki jijini Dar es Salaam na Bagamoyo kuwa mali ya serikali.

Kwa upande wa mshtakiwa wa pili, wakili huyo aliomba mshtakiwa alipe fidia ya Sh milioni 10  ya hasara aliyoishababishia TRA ambapo tayari alishalipa sh milioni moja.

Alidai kiasi kilichobaki kitalipwa kwa kipindi cha miezi 12 kwa kila mwaka  Sh 750,000.

Kwa upande wa mshtakiwa wa tatu, wakili huyo aliomba mstakiwa huyo alipe fidia ya sh milioni 300 kutokana na hasara aliyoisababishia TRA na tayari alishalipa Sh milioni 200.

Alidai, kwa mujibu wa makubaliano hayo, kiasi kilichobaki kitalipwa kwa kipindi cha miezi 10 kuanzia tarehe aliyoingia makubaliano na kila mwezi atalipa Sh milioni 10.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimuachia huru Mkurugenzi Mkuu wa Benki M (Tanzania), Sanjeev Kumar (63) na kumtaka kulipa fidia ya zaidi ya bilioni sita na faini ya Sh milioni mbili baada ya kukiri.

Mshtakiwa Kumar ametakiwa kuilipa fidia hiyo ndani ya miezi 24 ambapo mpaka sasa tayari ameshalipa milioni 690.

Akisoma adhabu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi alisema kuwa katika mashtaka hayo mawili mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh milioni moja kwa kila kosa. 

Alisema pia mshtakiwa atatakiwa kulipa fidia ya Sh 6, 039,103,579 ambapo atailipa kwa miezi 24,  kwa kila mwezi atalipa kiasi cha Sh milioni 222.8.

Kigogo wa Michezo, Michael Wambura alikiri makosa ya kujipatia jumla ya Sh milioni 100.9  na wakakubaliana na DPP kurejesha fedha hizo ndani kwa awamu ambapo Oktoba 7  alirejesha  Sh milioni 20,249,531.

Wakili maarufu, Dk Ringo Tenga na wakugenzi wenzake wameachiwa huru baada ya kuingia makubaliano na DPP ya kulipa Dola za Marekani 3,748,751.19, ndani ya miezi sita, kuiachia Serikali nyumba iliyopo Mikocheni na mshtakiwa wa sita kulipa Sh milioni 30.

Wakurugenzi hao wa Kampuni ya Six Telecoms, DK Tenga, Hafidh Shamte na Peter Noni na Noel Chacha Ofisa Mkuu wa Fedha wanatakiwa kulipa zaidi ya Sh bilioni tatu na Frank Mwalongo anatakiwa kulipa Sh milioni 30.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alisema makubaliano mengine ambayo mahakama inatakiwa kuzingatia ni kwamba washtakiwa wamelipa Sh milioni 150, Dola za Marekani 150,000 na Dola 3,585,115 zilizobakia washtakiwa kuanzia wa kwanza mpaka watano watalipa ndani ya miezi sita kuanzia Oktoba Saba.

Mshtakiwa Frank Mwalongo alilipa Sh milioni 35 alizokubali kulipa kama fidia na faini.

Hata hivyo katika mchakato huo wa kuomba msamaha na kukiri makosa, DPP ameweza kuwaondolewa washtakiwa wote Mashtaka ya kutakatisha Fedha na kubakia akiwashtakiwa kwa mashtaka mengine ya uhujumu Uchumi ikiwemo kuisababishia Serikali hasara.

Mshtakiwa mmoja tu Yasin Katera,  ndiye baada ya kusoma  upya hati ya mashtaka alishtakiwa  kwa shtaka la kutakatisha fedha na akalipa faini ya Sh milioni 100.

Watuhumiwa wengi bado wanaendelea kujadiliana na kufanya makubaliano na DPP jinsi ya kumaliza kesi za uhujumu uchumi zinazowakabili katika Mahakama mbalimbali.

Kwa watuhumiwa hao wote fedha zilizobaki ambazo Serikali inatakiwa kuzipata kutoka kwao kutokana na makubaliano waliyofikia zaidi ya bilioni 36.9 kwa kesi zilizoamuliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles