Na FERDNANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM
KATIKA jitihada zilizofanywa na serikali kuliwezesha Taifa kimaendeleo kwa ajili ya kuwainua vijana, kwa sasa imepiga hatua katika kukuza ajira kwa wananchi, hususan kwa upande wa vijana.
Hadi sasa takwimu zinaonyesha kuwa, katika taasisi ya Don Bosco kupitia Wizara ya Kazi na Ajira, ina zaidi ya vijana 3,440 katika mikoa yote waliopo kwa mafunzo.
Serikali kupitia Wizara ya Kazi na Ajira kwa vijana nchini haijawa nyuma katika kukuza ujuzi kwa vijana, hivyo imeendelea kuungana na taasisi hiyo ili kutoa mafunzo ya nadharia na vitendo katika fani mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.
Kupitia hotuba yake, Waziri wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, aliyoitoa mkoani Iringa hivi karibuni katika uzinduzi wa eneo la mafunzo kwa vijana wa Don Bosco, anasema serikali ina nia nzuri kabisa katika kusaidia vijana, hivyo ni hatua madhubuti ya maendeleo kwa jamii na kwa nchi kwa ujumla.
“Mpango wa serikali ni thabiti na endelevu, kwani una lengo stahiki kwa wananchi wake katika kutekeleza majukumu yao.”
Hata hivyo, Jenista anasema taasisi ya Don Bosco imekuwa ni tofauti na taasisi nyingine nchini katika utoaji wa huduma ya mafunzo kwa vijana, hivyo ni dhahiri kuwa serikali inamjali mwananchi katika nyanja zote.
Ikiwa ni mpango mkakati kwa vijana katika maendeleo, ni dhahiri kuwa vijana wanahitaji kuungwa mkono kwa asilimia kubwa kutoka kwa serikali ili kuweza kukuza uchumi wa viwanda na biashara kwa ujumla.
Hivyo jukumu na lengo stahiki la kutoa mafunzo ni kuwasaidia vijana wote wenye uhitaji wajifunze ili kuondokana na umasikini wa kuwa tegemezi.
Vilevile kitendo cha kuwa na elimu ya ujuzi wako binafsi humfanya mtu kufanya kile kinachostahili kwa wakati na si kusubiri ajira kama ilivyo kwa wasomi wengine wanaosubiri kuajiriwa na sio kujiajiri.
Dunia imebadilika na kuweka kipaumbele elimu, lakini kitendo cha kuwa msomi si kwamba ni lazima uajiriwe, bali uwe na uwezo wa kujiajiri mwenyewe kulingana na elimu uliyosomea.
Mara kadhaa inafahamika kuwa watu wengi mara baada ya kumaliza elimu ya chuo huwa ni watu wa kuzunguka na kutafuta ajira, hivyo kumfanya atumie muda mwingi wa kutafuta ajira, kumbe ni kutokujua tu, wakati unatafuta ajira unatakiwa kujishughulisha kwanza na kazi nyingine mbadala zinazowezekana kwa wakati huo kuliko kupoteza muda kwa kutafuta kazi kila siku.
Kwa kipindi hicho unachozunguka ungeweza kufanya kitu kikubwa ambacho kingekuwa na mafanikio mbadala kuliko hiyo kazi unayoihangaikia siku hadi siku, kwani ni kupoteza muda bure.
Ni watu wachache sana ambao huwa na mawazo chanya na mbadala, ambapo baada ya kumaliza elimu husika hufanya shughuli za ujasiriamali, huku wakiendelea kutafuta kazi bora kuliko ile anayofanya. Suala hapa huwa ni ubora wa kazi na si kazi!
Kutokana na kutokujiamini watu wengi huhitaji kuajiriwa zaidi na si kujiajiri wenyewe na hivyo huishia kutafuta kazi zaidi ya miaka kadhaa bila mafanikio.
Mpango mkakati wa utoaji wa mafunzo bure unaotolewa na taasisi hiyo ni fursa ya kipekee sana, kwani endapo utapata ujuzi hautahitaji uajiriwe, bali waweza kujiajiri mwenyewe.
Endapo vijana wengi watafunguka na kuchukua hatua, kujitambua na kulifanyia kazi hili, itawasaidia, pia itakuwa ni nguzo kwao katika kujipatia fursa wenyewe bila kuajiriwa.
Kuna usemi kuwa, hakuna kazi ambayo itakufuata ulipo, hivyo unatakiwa uchukue hatua kufanya kazi yoyote na si kuegemea kuajiriwa pekee. Njiani utakutana na kazi unayopenda au stahiki kwako.
Hiyo ni njia mbadala yenye mafanikio, badala ya kukaa kijiweni na kuanza kulaumu wala kujihisi ni mkosaji wa kazi, kwani serikali imekuwa ikiwasaidia zaidi vijana kujifunza fani mbalimbali.
Kupitia serikali, taasisi ya Donbosco imekuwa ni ya mfano wa kuigwa na taasisi nyingine kwa utoaji wa huduma bure kwa mafunzo ya vijana.
Hatua hii itafsiriwe ni kuwa chachu na mfano wa kuigwa na mashirika mengine nchini kujitokeza na kuwasaidia vijana wetu.
Anasema kuwa, ingawa taasisi hiyo ipo chini ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa vijana, isiwe ni kigezo kwa taasisi nyingine kutojitolea kikamilifu katika suala zima la kuwainua vijana na kuwapatia mafunzo ya aina mbalimbali.
Anasema vijana waliopo katika taasisi ya Don Bosco hupatiwa mafunzo mbalimbali yanayotolewa na taasisi hiyo ili kukuza ujuzi na maarifa, ili kukuza soko la ajira nchini.
Fani zinatolewa na taasisi ya Don Bosco zipo zaidi ya 8, ambazo zote hutolewa kwa vijana katika mikoa mbalimbali.
Mikoa ambayo hutoa mafunzo ya Don Bosco ni Dar es Salaam vijana 1,090, Shinyanga vijana 80, Iringa 770, Mafinga 180, Moshi 80 na Dodoma vijana 1,240.
Jenista anasema fani zinazotolewa kwa vijana hao kwa ujumla katika mikoa yote ni ushonaji wa nguo, ambapo huchukua muda wa mafunzo miezi 6 na una vijana zaidi ya 800, ufundi magari 302, useremala 250, uwashi 195, uchongaji wa vipuri vya magari na aluminium 158, ufundi bomba 295, ufundi wa umeme 160, Tehama 1010, kuweka tarazo na vigae vijana 120.