DOGO JANJA ANAPETA KATIKA MIKONO SALAMA YA TALE

0
746

Na RAMADHANI MASENGA

KATIKA miezi ya hivi karibuni kila wimbo aliotoa Dogo Janja umepokelewa vizuri. Mashairi yake na namna yake ya kuimba vinaonekana kuwakuna wengi.

Ila wakati ukijadili kipaji cha Dogo Janja usiepuke kusifu uwezo wa kuongoza wa Babu Tale. Babu Tale kama ilivyo kwa swahiba wake Saidi Fella ni mafundi wa kulea vipaji.

Wakati mwingine msanii akiwa katika kambi zao huwezi kuona ni wapi unafaa kuwasifia. Unaona msanii anang’ara.

Kila nyimbo anayotoa inakusisimua. Unaona yeye ni kila kitu. Unawasahau kina Fella na Babu Tale. Kosa kubwa! Kando na mtu kuwa na kipaji kikali, anahitaji usimamizi ili aweze kufikia matarajio.

Uongozi makini unaweza kumfanya msanii mahiri akawa mkali zaidi. Pia uongozi magumashi unaweza kumfanya msanii mahiri akaonekana wa kawaida sana.

Anza kuangalia sakata la Juma Nature na kina Luteni Kalama. Kuna kipindi hawa watu walikuwa ni kila kitu katika muziki wa Tanzania.

Kila kona walisifiwa. Kila mtu aliimba nyimbo zao. Kumbe wakati tukiwasifia wao, tulisahau maajabu makubwa yaliokuwa yakifanywa na Saidi Fella dhidi yao.

Wakajisahau. Wakaona uongozi unawanyonya na kuona wanaweza kufanya mambo yao wenyewe. Kiko wapi? Hakuna cha Luteni Kalama wala Juma Nature.

Kuna wakati ni lazima umsifie mtu hata kama humpendi. Babu Tale na Saidi Fella wanazungumzwa kwa mengi mabaya. Ila wazungumzaji wasisahau kusifu uwezo na umahiri wa hawa watu.

Dogo Janja atambaye leo ni yuleyule aliyefifia baada ya kuvimba kichwa na kwenda Mtanashati Entertainment. Ukiona kila siku Madee anatoa nyimbo mpya na inatamba usisahau kumsifia na Babu Tale.

Hawa watu wanafanya kazi nzito japo hatutaki kukubali. Diamond pamoja na usimba wake lakini ana heshima kubwa kwa hawa jamaa.

Inaonesha toka kitambo alisoma alama za nyakati na kujua uchawi wa Bongo Flava. Anawatumia na tunaona mafanikio yake.

Wasanii ni vema wakatambua kuwa na kipaji ni jambo moja ila kuwa na meneja makini ni jambo jingine. Meneja makini atakushauri, kukuonya na kukuelekeza nini ufanye kutokana na mazingira na wakati.

Hiki kitu wasanii wengi hawana ndiyo maana mbali na vipaji vyao vikali wanaishia kuwa wasanii wa kawaida tu mtaani.

Nani anapinga juu ya kipaji cha Young Dee? Tukiongea kwa kumuogopa Mungu, Young Dee ana kipaji kikubwa sana. Lakini yuko wapi?

Siku maajabu yakitokea na Young Dee akawa na meneja makini sampuli ya Sallam au Tale, watu watatafutana. Kijana  anajua kuimba, ana staili kali ila anakosa uongozi makini wa kumwambia nini cha kufanya na aishi vipi?

Meneja makini haishii kumtafutia msanii shoo tu. Atamshauri mengi na hata juu ya maisha yake binafsi. Wakati mwingine ukimuona Diamond anatulia na Zari, yape hongera mapenzi ila pia usiache kuwasifia walio karibu na Diamond.

Meneja mjanja humfanya msanii wake aonekane wa thamani na gharama. Ukiachana na Wema kisha ukawa na Zari ni zaidi ya kutoka kuishi Sinza na kuhamia Masaki!

Ukimuona Young Dee anatoka na Amber Lulu kisha kesho anakuwa na Gigy Money usilalamike tu ila muombee kwa Mungu ampate meneja makini atakayemwambia mtu anayekuwa naye ndiye anatayejenga taswira yake katika jamii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here