29.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

Dodoma yafanikiwa kuibua watoto wenye utapiamlo

Na Mwandishi Wetu – Dodoma

HALMASHAURI za Mkoa wa Dodoma zimefanikiwa kuongeza kiwango cha uibuaji wa watoto wenye utapiamlo hadi asilimia 79 kutoka Juni, mwaka huu kutoka asilimia 11  kutoka Desemba, mwaka jana.

Hayo yalisemwa jijini Dodoma jana na Mratibu wa Lishe Mkoa wa Dodoma, Herieth Carin wakati wa kikao cha tathmini ya hafua za lishe.

Alisema halmashauri nyingi zimetekeleza mkataba wa lishe  kipindi cha nusu mwaka yaani  Julai hadi Desemba, mwaka jana.

 “Halmashauri zimeongeza kasi ya uibuaji watoto wenye utapiamlo mkali kwa watoto wa chini ya miaka mitano na kutoa matibabu kwa watoto hao,” alisema Carin.

Alisema halmashauri  zilitoa mafunzo ya matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoa huduma za afya 223, wakiwemo 155 kutoka Mpwapwa, Kongwa (21), Chamwino (19), Bahi (5), Dodoma Jiji (12), Chemba (2), Kondoa (3) na Kondoa Mji (5).

Alisema zilifanya ufuatiliaji wa ukusanyaji wa takwimu kwa kuandaa na kusambaza fomu maalumu za kukusanyia taarifa kwa wahudumu ngazi ya jamii pamoja na vituo vya kutolea huduma.

Carin alisema kuna baadhi ya halmashauri zilitoa fedha kidogo tofauti na zilivyotenga kwenye bajeti yake kutekeleza afua za lishe ili kupunguza athari za kilishe kwa watoto hao.

Kati ya halmashauri hizo, Chamwino iliongoza kwa kutenga na kutumia fedha nyingi kwa ajili ya afua hiyo, ilitenga Sh milioni 22.4 na kutumia sh milioni 22.3 sawa na asilimia 99 ya fedha hizo.

“Halmashauri ya Bahi ilitenga Sh milioni 54.5 na ikatumia Sh milioni 44.6 sawa na asilimia 82, wakati Mpwapwa ilitenga Sh milioni 72.1 na ikatumia Sh milioni 55.3 sawa na asilimia 78.

“Halmashauri ya Kondoa Mji ilitenga Sh milioni 32.3, lakini ilitumia Sh milioni 19.02 sawa na asilimia 59, wakati Kongwa ilitenga Sh milioni 86.8 na kutumia Sh milioni 50.02 sawa na asilimia 58 ya bajeti.

 “Kondoa ilitenga Sh milioni 76.2, lakini ikatumia Sh milioni 30.7 sawa na asilimia 40, wakati Jiji la Dodoma lilitenga Sh milioni 147.03, lakini lilitumia Sh milioni 54.7 sawa na asilimia 37, vile vile Chemba ilitenga Sh milioni 53.5 ikatumia Sh milioni 11.5 sawa na asilimia 21,” alisema Carin.

Alisema halmashauri kupitia idara zake mtambuka za lishe kama vile Idara ya Maendeleo ya Jamii, Elimu, Kilimo na Ufugaji, ziliendelea kutoa elimu kwa jamii namna bora ya kuinua na kuongeza kipato ngazi ya kaya kwa kutumia Tasaf na mifuko ya vijana na wanawake.

Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge aliwapongeza wakurugenzi ambao walitenga fedha katika bajeti zao na wakatumia kutekeleza afua za lishe kwa asilimia kubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,701FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles