23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, June 4, 2023

Contact us: [email protected]

DMDP awamu ya pili kumaliza kero za miundombinu Segerea

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, amesema awamu ya pili ya ujenzi wa miundombinu ya Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP) itamaliza kero ya miundombinu kwa wakazi wa jimbo hilo.

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, akizungumza na Diwani wa Kata ya Kipawa, Aidan Kwezi, baada ya kukagua ujenzi wa daraja linalotenganisha jimbo hilo na Ukonga. Kulia ni Msimamizi wa mradi huo kutoka Tarura Ilala, Injinia Sillo Joseph.

Bonnah ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Kata za Segerea, Vingunguti, Liwiti na Kipawa.

“Jimbo la Segerea lina changamoto kubwa ya barabara lakini kupitia mradi wa DMDP awamu ya pili tuna uhakika sasa kero zote zitakwenda kumalizika. Tunamshukuru sana rais, Waziri wa Tamisemi na Waziri wa Fedha kwa kupeleka haraka mradi huu,” amesema Bonnah.

Aidha amesema kupitia Sh milioni 500 zilizotolewa kwa kila jimbo wataendelea kuboresha miundombinu ikiwemo barabara ya Uwanja wa Ndege Karakata yenye urefu wa kilomita 1.5 ambayo pia wanaangalia uwezekano wa kuiingiza DMDP iweze kutengenezwa kwa ubora zaidi.

Akiwa katika Kata ya Vingunguti Bonnah amesema barabara iliyoanza kujengwa kuanzia eneo la Scania hadi darajani sasa itaendelea kutengenezwa kwa kiwango cha lami hadi Barakuda baada ya Serikali kuongeza Sh bilioni 3.1 kumalizia kipande kilichobaki.

Msimamizi wa mradi huo kutoka Tarura – Ilala, Injinia Sillo Joseph, amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 2.83 inayogharimu Sh bilioni 6.02 ilianza kujengwa Novemba mwaka jana na inatarajiwa kukamilika Oktoba 27 mwaka huu.

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, akizungumza na Diwani wa Kata ya Segerea, Robert Manangwa, baada ya kukagua Kituo cha Daladala Segerea ambacho kimewekwa taa kupitia fedha za mfuko wa jimbo. Kulia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Migombani, Samwel Binagi na kushoto ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Segerea, Elgius Mulokozi.

Aidha katika Daraja linalojengwa Kipunguni Banana, Injinia Joseph amesema linagharimu Sh milioni 250 na linatarajiwa kukamilika mwezi ujao.

Naye Diwani wa Kata ya Kipawa, Aidan Kwezi, amesema tayari wamepokea Sh milioni 200 za ujenzi wa shule mpya ya Minazi Mirefu ambazo zimetumika kujenga madarasa kumi na kwamba wanatarajia kupokea tena Sh milioni 300 za ujenzi wa madarasa ya ghorofa.

Amesema pia wamepokea Sh milioni 50 za ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya Msingi Majani ya Chai na kwamba ujenzi wa ukuta nao umefikia hatua nzuri.

Diwani wa Kata ya Liwiti, Alice Mwangomo, amesema wana mpango wa kujenga shule ya sekondari na tayari Sh milioni 400 zimetengwa huku Sh milioni 300 zikitoka Serikali Kuu na Sh milioni 100 zikitolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Naye Ofisa Mtendaji wa Kata ya Segerea, Elgius Mulokozi, amesema walipokea Sh milioni 45 zilizotolewa kupitia fedha za Mfuko wa Jimbo ambapo Sh milioni 32.4 zimetumika kuweka taa katika Stendi ya Segerea ambayo awali haikuwa na taa.

Amesema fedha zilizobaki Sh milioni 16.7 watatumia kuziba mashimo na tayari wametangaza zabuni kwa ajili ya kazi hiyo.

Mwaka jana kata hiyo ilipokea Sh milioni 25 kutoka katika Mfuko wa Jimbo ambazo zilitumika kukarabati Shule ya Msingi Maendeleo ambayo iliezuliwa paa pamoja na kupaka rangi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,284FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles