33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

DKT. TIZEBA: ‘SERIKALI HAINA TAKWIMU ZA MAZIWA NCHINI’

Na AMINA OMARI-TANGA

SERIKALI haina takwimu halisi za maziwa yanayozalishwa nchini, imeelezwa.

Hayo yameelezwa juzi na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, wakati wa ziara yake ya siku moja kutembelea kiwanda cha kuzalisha maziwa cha Tanga Fresh.

Alisema mfumo dhaifu wa ukusanyaji wa maziwa nchini, ndio umesababisha viwanda vingi vya maziwa kufungwa kutokana na kukosa malighafi hiyo.

“Mfumo wa kutoa ripoti za maziwa una kasoro, lakini ukiuliza unaambiwa ni mfumo wa kimataifa.

“Huo mfumo wa kimataifa wanaousema una taarifa zinazohusu maziwa yaliyopitia viwandani wakati kuna mengi ambayo yanauzwa huko mitaani bila kupitia kwenye mfumo huo wa kimataifa.

“Katika kumaliza changamoto hiyo, Serikali ipo kwenye mazungumzo na Shirika la Maendeleo la IFAD kwa ajili ya kutukopesha Dola za Marekani milioni 34 ili tuweze kutengeneza mfumo wa ukusanyaji wa maziwa.

“Mfumo huo kwa majaribio utaanza katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Njombe, Iringa na Mbeya kwa kuhakikisha wafugaji wanasaidia kukusanya maziwa na kuweza kuyafikisha kiwandani yakiwa salama,” alisema Dk. Tizeba.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Tanga Fresh, Michael Karata, alisema changamoto kubwa inayaoikabili sekta ya maziwa ni ukosefu wa mitamba bora pamoja na malisho.

“Wakati wa kiangazi, uzalishaji unashuka kutokana na kutokuwa na malisho ya uhakika kwa mifugo ili iweze kutoa maziwa.

“Kwa hiyo tunaiomba Serikali itujengee kiwanda cha kuchakata nyasi ambazo zitaweza kuhifadhiwa na kutumika katika misimu ya kiangazi pamoja na kupatiwa mitamba ya bei nafuu ili kuongeza uzalishaji katika sekta yetu ya maziwa,” alisema Karata.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Ngombe wa Maziwa Nchini (TDCU), Hamid Mzee, alisema pamoja na sekta hiyo kuchangia katika pato la Taifa, bado Serikali haijatoa kipaumbele katika maziwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles