25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Tulia: avunja ukimya

Dk. Tulia Ackson
Dk. Tulia Ackson

Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam

SIKU mbili baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuahidi kufanyika maridhiano kati ya uongozi wa Bunge na wabunge wa upinzani katika kikao kijacho kinachotarajiwa kuanza Septemba 6, mwaka huu, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson amesema hataki kuwasikia wabunge wa upinzani wala kuwawaza.

Kauli hiyo ya Naibu Spika huenda ikazidi kutonesha kidonda hasa baada ya Bunge la Bajeti lililofanyika Mei mwaka huu kuacha majeraha kutokana na wabunge wa upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia vikao vyote vilivyoendeshwa na kiongozi huyo.

Juzi wakati akihojiwa kupitia kipindi cha Funguka kinachorushwa na Kituo cha Luninga cha Azam, Spika Ndugai,  alisema anatafuta mbinu ya kuweka sawa mambo hayo kwa kufanya maridhiano  ikiwemo kushirisha maspika wastaafu.

Akizungumza na MTANZANIA juzi katika mahojiano maalumu ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Dk. Tulia alisema hapendi kuwawazia wabunge hao wa upinzani.

“Kwa kuwa Spika yeye kazungumza siwezi kucomment chochote kwa sababu sipendi kuwawazia wabunge hao,”alisema.

Alipoulizwa kwamba ni kwanini migogoro ilizidi wakati yeye akiwa anaendesha vikao, alisema alichokuwa anafuata ni kanuni na kwamba malalamiko hayawezi kukosekana.

“Nashangaa wengine wanasema kuendesha vikao ni mpaka uwe na uzoefu…unajua zile kanuni hata ukipewa uendeshe wewe ukishazielewa hazihitaji uzoefu wowote. Kulalamika kuwa nawapendelea ni jambo la kawaida.

“Kwa mfano siku iliyotokea vurugu wakati wabunge wa upinzani wanadai kutorushwa matangazo ya Bunge live, aliyekuwepo kwenye kiti alikuwa ni mwenyekiti ambaye ni mzoefu wa siku nyingi na ni yeye aliyepeleka majina yao kwenye Kamati ya Maadili, sasa sidhani kama hiyo ni hoja,”alisema Dk. Tulia

Alieleza kushangazwa kwa kitendo cha wabunge wa upinzani katika barua yao waliyomwandikia Spika kwamba hawana imani naye, huku akihusishwa na fedha zilizorejeshwa serikalini.

“Katika ile barua walieleza sababu nyingine kuwa hawana imani na mimi, wakanihusisha na zile Shilingi bilioni 6 zilizorejeshwa serikalini wakati sheria na utaratibu upo wazi kwa sababu Spika au Naibu Spika hauhisiki na masuala ya fedha bali anayehusika ni Katibu wa Bunge.

“Kwa hiyo ni jambo la kushangaza kwamba Naibu Spika karudisha fedha, mimi si mshika mafungu lakini pia ni namna watu walivyopokea huwezi kuwazuia wanavyokuwazia,” alisema.

Akizungumzia kauli ya Spika Ndugai kwamba kwa kuwa Bunge la 11 lina wabunge wapya wengi na kwamba kuwaongoza kunahitaji uvumilivu mkubwa alisema: “Nisingependa kuongelea kauli ya Spika…lakini uvumilivu wa mtu kutakiwa akae hadi mara 11 halafu ameendelea kusimama ni uvumilivu gani huo?,” alihoji.

Pamoja na mambo mengine alisema wakati wabunge wanawake wa Ukawa walipojitoa kwenye  Chama cha Wabunge Wanawake (TWPG), alitukanwa tusi kubwa lakini alinyamaza.

Mei 5, mwaka huu wakati akichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria, Mbunge wa Ulanga Mashariki, Gudluck Mlinga (CCM), alidai kuwa ili kuwa mbunge wa viti maalumu Chadema lazima uwe ‘baby’ wa mtu.

“Laiti ungeona Hansard tusi walilonitukana siku ile, actually Mlinga hajatukana lakini ulisikia nikilalamika mahali kwamba nimetukanwa? wao wanaongee vibaya…watukane, mimi bado ni kiongozi wao na siwezi kuanza kuwakasirikia itakuwa sasa nashindwa kuwaongoza mimi ni kama mzazi wao,” alisema Dk. Tulia.

Alisema kitendo cha watu kudai kwamba anafanya upendeleo bungeni ni changamoto ya kawaida, kwa sababu hata katika mabunge ya Jumuiya ya Madola malalamiko ya aina hiyo yapo.

“Pale bungeni  wako wabunge 389, hawa ni wengi sana wote hawawezi kupata nafasi ya kuongea. Kwa mfano uliomba nafasi jana ukapewa ukaomba leo, hata ukisimama mara 11 katika hali ya kawaida huwezi kupewa kwa sababu wako wengi ambao hawajachangia.

“Kama kiongozi naona ni sehemu mojawapo ya kusimamia jamii ni changamoto na itaendelea kuwepo kwa miaka mitano,”alisema Dk. Tulia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles