23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Tulia: Bunge halitataja ugonjwa wa mtu

RAMADHAN HASSAN

NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, amesema kuwa ugonjwa wa mtu ni siri, hivyo hakuna mahali Bunge litatangaza kuwa mtu fulani amekufa na ugonjwa fulani.

Kauli hiyo aliitoa juzi bungeni wakati akifafanua kuhusu vifo vya wabunge vilivyotokea hivi karibuni na watu kujaribu kuhusisha na ugonjwa wa corona.

“Waheshimiwa wabunge sisi sote ni viongozi, tunafahamu ugonjwa wa mtu ni siri yake yeye peke yake, akitaka sana yeye na daktari. Sasa hatuwezi kufika mahali tukalazimishana kwamba mtu aseme ugonjwa wake ni nini ama mtu mwingine amsemee mtu mwingine kwamba amekufa na ugonjwa gani.

“Wale walioumwa hata na virusi vya corona wametangaza wao wenyewe, hakuna mahali Serikali imesema nani amekufa na ugonjwa gani kwa sababu kila mtu ana ugonjwa wake na ugonjwa ni siri ya mtu.

“Kama ameamua kusema hilo ni suala lake, kama hakusema mkakuta mauti yamemchukua ameondoka nayo siri yake yeye na daktari, haimhusu mtu mwingine.

“Kwa hiyo hakuna mahali tutafika kama Bunge kuanza kutangazia mbunge fulani amekufa na kifo fulani, hilo halitowezekana, kwa hiyo likae hivyo, nadhani tutakuwa tumefuata miongozo yote ambayo inawataka wenzetu kwenye eneo la afya kufanya hivyo nasi tusingetaka kuingia kwenye eneo hilo,” alisema Dk. Tulia.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wabunge kuhakikisha wanafuatilia kwa umakini hotuba za Rais Dk. John Magufuli ili waweze kujua kinachoendelea.

“Unapokuwa umechukua mambo yaliyozungumzwa nje ya muktadha, unapelekea wewe mwenyewe kuanza kujikosesha heshima na pia kumkosea heshima kiongozi wetu mkuu wa nchi. 

“Kwa hiyo tusikilize kwa makini yale anayoagiza na tufuate hayo tusijifanye kila mtu sasa ni mwamba kwenye eneo lake na yeye basi anaweza kuwa rais hapana,” alisema Dk. Tulia. 

Alisema nchi ina rais mmoja na anavyotoa maelekezo yeye ndiyo kiongozi wa nchi na amepewa dhamana kwa kipindi hiki chote yeye peke yake.

Dk. Tulia alisema kuwa hakuna mtu mwingine, sehemu nyingine anaweza na yeye akajifanya ni rais akaanza na yeye kutoa maelekezo yake.

“Akishasema rais ameshasema na amemaliza mpaka atakapobadilisha yeye. Na asemacho nafikiri sisi kama wabunge tunafahamu anachozungumza rais ni sheria,” alisisitiza Dk. Tulia. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles