Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Stergomena Tax (Mb.) amewasili katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam na kupokelewa na Naibu Waziri, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.), Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine pamoja na baadhi ya watumishi wa Wizara.
Dk. Tax aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Oktoba 2, 2022 na kuapishwa tarehe 03 Oktoba 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo Dk. Tax amechukua nafasi ya Balozi Liberata Mulamula baada ya Rais kufanya mabadiliko madogo kwenye Baraza la Mawaziri.
Mara baada ya kuwasili Katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, leo Jumatatu Oktoba 2, 2022 Dk. Tax amesema atafanya kazi kwa ushirikiano na watumishi wote wa Wizara katika kila ngazi ili kuhakikisha kuwa malengo ya Wizara yanatekelezeka.
“Nipo tayari kufanya kazi na nyinyi, na kujifunza kutoka kwenu ili niweze kutekeleza majukumu yangu….. taasisi yoyote ili iweze kufanikiwa lazima kufanya kazi kwa pamoja na ushirikiano,” amesema Dk. Tax.