29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

DK. SLAA: WASIPOKUJA NA AJENDA MPYA, UPINZANI UTAFUTIKA KABLA YA 2020

Na ELIZABETH HOMBO


DK. Willibrod Slaa ni miongoni mwa wanasiasa waliojizolea umaarufu kutokana na utendaji wake tangu akiwa Mbunge wa Karatu na baadaye Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

 

Mwanasiasa huyo machachari, Septemba mwaka 2015 wakati wa Uchaguzi Mkuu alijiweka kando na siasa baada ya kutofautiana na chama chake akidai kutoridhishwa na kitendo cha kumpokea Waziri Mkuu (Mstaafu), Edward Lowassa ambaye chama chake cha CCM kilimkata jina lake katika hatua ya awali katika                         kinyan’ganyiro cha kuwania kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Kutokana na hilo, amekuwa katika taswira tofauti ambazo zinatoa maelezo yasiyofanana miongoni mwa wafuasi wa masuala ya siasa.

 

Wapo wanaomwona kama mwanasiasa shupavu na mkombozi wa jamii ya Watanzania kutokana na juhudi zake alizofanya kwenye mapambano dhidi ya ufisadi nchini.

 

Pia amekuwa kipenzi kwa wafuasi wa siasa za upinzani huku wengine wakimwona kama mwanasiasa aliyepoteza mwelekeo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi akidaiwa kuwa amerubuniwa na CCM ili kuikwamisha Chadema.

 

Wiki iliyopita MTANZANIA ilifanya mahojiano na Dk. Slaa kwa njia ya barua pepe akiwa nchini Canada ambapo alizungumzia masuala mbalimbali yanayohusu siasa za Tanzania na fikra zake namna ya mwenendo wa siasa za Tanzania zinavyokwenda.

 

Yafuatayo ni mahojiano hayo:

MTANZANIA: Nini tathmini yako kuhusiana na utendaji wa Rais Dk. John Magufuli tangu aingie madarakani?

 

DK. SLAA: Kwanza napenda kuchukua nafasi hii kuwasalimia Watanzania wenzangu. Ni muda mrefu tangu tumewasiliana kwa njia ya makala. Naamini kwa ujumla mko salama salimini.

 

Nikirudi kwenye swali la msingi. Itoshe tu kusema, kwa muda mrefu Watanzania walitamani  na kumwomba Mungu awapatie Rais mwenye uamuzi, Rais anayekuwa baba mwema katika nyumba, mwenye kuchukua hatua ili kudhibiti na kusimamia masuala mbalimbali ndani ya kaya yake.

 

Ni baba wa ajabu ambapo vijana wake wanarudi nyumbani muda wanaotaka, wanakunywa kupitiliza au kuvuta bangi, hawafanyi kazi yoyote ndani ya familia kwa manufaa ya familia. Ni baba wa ajabu zaidi wakati anaona mali za familia zinatapanywa na baadhi ya wanafamilia naye amekaa kimya.

 

Nimeona nianze na mfano huo ambao kila Mtanzania atauelewa. Kwa takribani miaka 20 Watanzania katika ujumla wao, lakini hasa vyombo vya habari, wanasiasa hasa wa upinzani na wananchi waliokuwa na mwamko kiasi  tumekuwa tukipiga kelele kuhusu masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na uzembe na kutokuwapo uwajibikaji serikalini.

 

Tumekuwa tukipiga kelele dhidi ya ukwepaji mkubwa wa kodi na ushuru mbalimbali. Tumekuwa tukipiga kelele dhidi ya dawa za kulevya baada ya kuona vijana wetu wakiangamizwa na kundi la watu lisilojali uhai wa vijana wengine, wao wakitumika kama punda kusafirisha dawa hizo kwa njia mbalimbali.

 

Wengine  walipasukiwa na kete hizo na kulazimika kufanyiwa upasuaji. Vijana  wengi walikamatwa nchi mbalimbali kama China, Afrika Kusini na hata jirani zetu Kenya. Wengi wao hadi sasa wanaozea kwenye magereza ya nchi hizo.

 

Ndani ya siku 100 ya uongozi na utawala wake alichukua hatua maridhawa, ikiwa ni pamoja na “ kutumbua” wahusika. Kitendo hicho cha Rais kiliungwa mkono kwa shangwe na vigelegele na Watanzania wengi wenye nia njema na Taifa letu.

 

MTANZANIA: Pamoja na hilo, lakini sasa hali hiyo imebadilika  huku wengine wakimkosoa kutokana na matamko ambayo yanatajwa kuwa ni kukurupuka, hili unalizungumziaje?

 

DK. SLAA: Nafikiri kwanza tukubaliane kuwa hakuna nchi hata moja ambapo kiongozi atakubalika na watu wote kwa asilimia 100. Wako  ambao masilahi yao yataguswa kwa namna mmoja au nyingine. Hao ni wazi watapiga kelele.

 

Kwa bahati mbaya wana masilahi duniani kote ndio wenye uwezo kwa maana ya nafasi na vyeo vyao au fedha zao. Kelele zao kutokana na uwezo wao zina mwangwi mkubwa. Lakini hawa wanaweza kuwa ni kundi dogo sana lenye masilahi binafsi wala wanachopigania si masilahi ya umma mpana.

 

Kuhusu suala la njaa, kwa uzoefu wangu wa miaka 20, kuwa na mvua kusiwe na mvua kuna kikundi cha watu ambacho siku zote kimekuwa na ukosefu wa mlo hata wa siku. Sababu ziko nyingi, si muda mwafaka kuzijadili hapa.

 

Lakini huwezi kusema kuna njaa, wakati kuna mikoa inasaza chakula. Kuna ukame kwenye mikoa kadhaa, lakini kwenye mikoa mingine mvua zinanyesha hadi mafuriko. Tatizo hapa ni la mgawanyo wa chakula, si tatizo la “ Njaa kama Taifa”.

 

Wanaosema kuwa Rais kakurupa kwa kusema kuwa hakuna njaa, nadhani Rais alikuwa makini sana kujua ukweli na kuwa tatizo la ‘distribution (utawanyaji) si tatizo lenye hadhi ya kutangaza ‘hali ya njaa’ kwa nchi nzima.

 

Utakubaliana na mimi kuwa baada ya Rais kusisitiza, hakuna taarifa yoyote ya Serikali au hata ya NGO na wanaharakati kuwa kuna Mtanzania amekufa kwa njaa. Nampongeza  Rais kwa usimamiaji wa kauli yake ambayo tuliikosa muda mrefu.

 

Watanzania hebu tujiulize, miaka yote tulipotangaziwa ‘ hali ya njaa’ familia gani ilipelekewa chakula cha kujitosheleza, kama si vigaloni na kilo za maharage! Hii ilikuwa ni kuwadanganya Watanzania na kuwapa matumaini ambayo hata siku moja hayakutekelezwa.

 

Kwangu mimi hii ni siasa ‘uchwara’ isiyo na ajenda, ambayo hukimbilia kusahihisha tu kauli za viongozi. Kwa bahati mbaya siasa ikikosa ajenda endelevu hayo ndiyo matokeo husubiri matukio na kuyageuza kuwa ajenda. Ndiyo maana kwa mwaka mzima na zaidi sasa hakuna ajenda mbadala.

 

Hivyo bila kuingia kwa undani zaidi, niseme kuwa ni kweli kwenye mitandao kuna kauli kadhaa za kumpinga Rais. Hizi ni siasa za mitandao. Wananchi walio wengi walimwelewa Rais, kuwa kufanya kazi ni kutunza na kukuza utu wetu kuliko ahadi hewa za kulishwa.

 

Hata baba wa familia asiyeweza kulisha familia yake hukosa heshima kwenye jamii. Alichosisitiza kwa vitendo Rais, ni kuwa watu walime kwenye mabonde, kando kando ya mito na ardhi oevu kwa mujibu wa sheria ili kila familia iweze kujihami.

 

Mahali pengine mvua za masika zitakapoanza watu wapande mazao ya muda mfupi na yenye kustahimili ukame. Kwa muda mrefu mimi mwenyewe nimekuwa nikipiga kelele kuwa Tanzania si nchi ya kuomba chakula, bali ni nchi ya kupeleka misaada nje na kuuza chakula nje.

 

Kwa kuwa Bunge la Bajeti ndio linatazamiwa kukaa nashindwa kuzungumzia mwelekeo mpana wa kiuchumi na kimaendeleo kwa kuwa sijaona hata Rasimu ya Bajeti yenyewe ya 2017/2018.

 

Hata hivyo Bajeti ya 2016/2017 ambayo kuna malalamiko kuwa fedha zilizotoka ni kama asilimia 34 tu.  Kwa uzoefu wangu, Rais ameleta mabadiliko makubwa sana. Anaiondoa nchi kutoka kwenye uozo, analirudisha Taifa kwa wananchi badala ya kundi dogo la viongozi na wafanyabiashara.

 

Amewabana wakwepa kodi. Hivyo, ni dhahiri kabisa kuwa uchumi katika ujumla wake utasuasua. Hili ni jambo la kawaida baada ya kila uchaguzi. Lakini ni mbaya zaidi kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa si wote wanaopenda mabadiliko aliyoanzisha Rais.

 

Ni kweli pia kuwa hatua zingine zilizochukuliwa na Rais na Serikali yake imeondoa fedha nyingi kwenye mzunguko, hivyo hali ya ukata ambayo watu wadogo wanaiona ni matokeo. Lakini kwa bahati mbaya zilikuwa hatua za lazima, kama ambavyo ukitaka kupona jipu, dawa pekee ni kuliminya hadi utoe kabisa mzizi wake. Hakuna njia fupi.

 

Ni imani yangu kuwa Bajeti ya pili ya JPM itapunguza maumivu hayo kwa kuelekeza fedha nyingi zaidi kwa maeneo ambayo yatawanyanyua zaidi watu wadogo. Aidha nategemea bajeti ya pili kujielekeza kwa kiwango kikubwa kujenga msingi wa Tanzania ya Viwanda.

 

Tanzania ya viwanda ina sura kuu mbili. Viwanda vikubwa vitakavyotokana na rasilimali chuma, makaa ya mawe na madini ya aina mbalimbali. Ni lazima twende kwenye Value Added, badala ya kufikiria zaidi kusafirisha nje raw materials ( malighafi). Value added Industrial approach ndio pekee itakayotengeneza ajira nyingi kwa vijana wetu.

 

Ni imani yangu kuwa Bajeti ya 2017/2018 itatoa msingi wa Tanzania hiyo tunayoitamani.  Sura ya pili ni ya Agro Industries, yaani viwanda vinavyoongeza thamani ya bidhaa zetu za kilimo. Ili hiyo iwe ni lazima kwanza tuimarishe kilimo chetu. Ninaona aibu nikiona mbegu za maboga zinauzwa Supermarket wakati sisi hata kuyathamini tu hatuyathamini.

 

Uturuki wanauza matunda ya mti unaitwa ‘fig’ ukiyatazama kwa macho unaweza usitamani kuyala. Lakini sisi tumekaa tu, hakuna anayefanyia utafiti namna ya kutumia rasilimali zetu. Hili si la Rais ni letu sote Watanzania.

 

Kupanga ni kuchagua. Hata kama Bajeti ya 2016/2017 kwa sehemu kubwa haikutekelezwa, lakini Rais kwa mamlaka aliyopewa na sheria za fedha, fedha zote zilizookolewa kutoka kwenye vianzio mbalimbali ameelekeza kwenye miradi mikubwa ambayo ndio uhai wa Taifa.

 

MTANZANIA: Unazungumziaje kitendo cha Rais Magufuli kuzuia mikutano ya vyama vya siasa?

 

DK. SLAA: Wakati mwingine tusipende kusingizia kwa madhaifu yetu.  Ninachojua ni kuwa baada ya tangazo lilikwenda kwenye sura ya ‘Civil disobedience’(kugomesha wananchi kukataa kutii sheria za nchi).   

 

Polisi kwa kutumia sheria zilizoko walichukua hatua na kudhibiti. Kugomesha wananchi au kuwafanya wasitii sheria ni kosa kwa mujibu wa sheria zilizoko. Wala Rais hajatunga hizo sheria. Hebu yachambue matamko yaliyotolewa na chama kimoja kikuu cha upinzani. Hakuna Taifa duniani litaruhusu Civil disobedience.

 

Lakini naona tumesimamia tu propaganda kuwa JPM kazuia mikutano ya hadhara. Waliozuia mikutano ni vyama vilivyotoa matamko ya kuitisha Serikali kwa kutaka kugomesha wananchi. Walisahau tu kuwa Serikali ndiyo iliyoshika upande mkali wa shoka (panga). Hivyo kwa hili vyama vijilaumu vyenyewe na wananchi wavilaumu vyama vilivyosabasisha hali hiyo.

 

MTANZANIA: Unazungumziaje kitendo cha aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye kutishiwa bastola na askari kanzu?

 

DK. SLAA: Sina sababu ya kulizungumzia hili kwa sababu limekwisha kutolewa ufafanuzi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba. Kukosa uadilifu kwa kawaida ni suala la mtu mmoja mmoja si la Serikali.  Kama amekwisha kujulikana anapaswa kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

 

MTANZANIA: Unauzungumziaje mgogoro unaofukuta ndani ya CUF?

 

DK. SLAA: Nadhani suala la CUF sina sababu ya kulijibu.  CUF ni chama cha siasa na pande zote zimekwisha kusema mara kadhaa waachiwe mgogoro wao. CUF ni chama kikubwa, kina wanachama wengi pande zote mbili za Muungano. Wanaweza kuyamaliza bila kuingiliwa.

 

MTANZANIA: Unadhani JPM ametekeleza kwa kiwango gani yale uliyokuwa ukiyategemea?

 

DK. SLAA: Kama ninavyosema siku zote, yale ya kundi ambalo halihitaji fedha ameyatekeleza yote kwa asilimia 99.9. Haya ni pamoja na kurudisha uwajibikaji serikalini, kuchukua hatua kali dhidi ya rushwa, wizi wa mali za umma na uwindaji haramu, na kudhibiti dawa za kulevya.

 

Hivyo, hatua zote zimechukuliwa, lakini zinapaswa kuwa endelevu. Kwa bahati mbaya mchwa wengine waliopenya mpaka ndani ya Ikulu na Serikali na huwezi kufagia Serikali nzima kwa siku mmoja.

 

Lakini kwa jinsi Rais hayumbi na wala hayumbishwi, nina hakika atafikia malengo na kurudisha Taifa kwenye misingi ya Tunu za Taifa ya uwazi, ukweli, uadilifu, kuheshimiana na kuthaminiana na hasa kujali utu. Nchi ilivyokuwa lazima tukubali mchezo wa saa ya ‘Pendelum’ kwa wale vijana wa zamani wanaokumbuka hizo saa.

 

Hujazwa kwa cheni na ikijaa huenda kulia, kushoto mara kadhaa kabla ya kutulia katikati. Hii ndio hali ambayo JPM kila siku anaiita ‘Transition’( kipindi cha mpito). Tutafika tu, tunatakiwa kuwa wavumilivu na wenye uzalendo wa kweli na nia njema ya kufikisha Taifa mahali pazuri. Hii inahitaji kuweka pembeni masilahi yetu binafsi kama mtu mmoja mmoja, viongozi wa Serikali au hata wa kisiasa.

 

Matarajio ya kiuchumi popote pale hayatekelezwi ndani ya mwaka mmoja. Ndio sasa tumemaliza Bajeti ya kwanza. Ndio maana nimesema nahifadhi mawazo na maoni yangu hadi baada ya kuchambua Bajeti ya 2017/2018. Lakini hatua zilizochukuliwa kujenga msingi wa uchumi hadi sasa zimeniridhisha kwa kiasi kikubwa.

 

MTANZANIA: Unadhani mwenendo huu wa JPM utasaidia upinzani kuingia Ikulu 2020?

 

DK. SLAA: Kama nilivyorejea mara kadhaa upinzani makini utaingia Ikulu kwa ajenda mbadala. Ajenda makini yenye kuwalenga wananchi moja kwa moja katika kuwatoa kwenye kero zao mbalimbali. 

 

Hadi sasa ninachoona ni kurukia kauli za JPM, lakini kauli si ajenda na hatupeani maksi kwa kuzungumzia usahihi wa lugha. Wako wanaotazama usahihi wa lugha na mahali pa kutazama usahihi huo.

 

Kimsingi darasani au kwenye uandishi wa vitabu.  Aidha kumtuhumu JPM kukiuka Katiba na sheria nayo haina tija. Wote wanaomtuhumu wanajua kuwa wakiambiwa waonyeshe kifungu mahususi alichokiuka yeye mwenyewe katika utendaji wake hawana majibu ya kuridhisha.

 

Wanajua kabisa kuwa kama Rais angelikuwa amevunja Katiba na sheria kama wanavyodai kuna ‘Reliefs’ mahakamani zinazoitwa ‘Prerogative Orders’, za Certiorari, Prohibimus na Mandamus”. Haya ni maneno ya kilatini yenye kutumika katika sheria kuelekea nafuu anazoweza kupata mwananchi au taasisi kupitia mahakamani.

 

Mbona hawajazitumia hata siku moja. Kama Dk. Slaa nikiwa Mbunge wa Karatu (kwa msaada wa wakili Dk. Mvungi RIP) tuliweza kumzuia Rais Mkapa kuvunja Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, leo wana timu kubwa ya mawakili wameshindwa nini kwenda mahakamani kuweka hizo Prerogative Orders? 

 

Hivyo mimi sijaona mwenendo wa JPM unaosaidia kuingiza upinzani Ikulu. Isitoshe kama hawatakuja na ajenda makini na mkakati ulioandaliwa unaowatoa wananchi hapa walipo kwenda kwenye raha, upinzani unaweza kufutika kabla ya 2020.

 

Dalili ya kwanza ni upinzani kukimbia agenda zake muhimu za ufisadi na wizi wa mali ya umma na pia kugeuka kuwa kichaka cha mafisadi na watuhumiwa wa dawa za kulevya. Chama cha upinzani kinapaswa kisiwe na doa wala cha kunyooshewa kidole wakati wowote ule.

 

Mwalimu Nyerere alipata kusema kuwa; ‘ Mke wa Mfalme si tu akamatwe ugoni, bali hatakiwi hata kudhaniwa tu’. Ili uweze kumnyooshea mkono mtu lazima kwanze uwe safi na si tu ujiamini kuwa safi bali na watu wakuone hivyo pia.

 

MTANZANIA:  Nini matarajio yako kisiasa na pengine unarudi lini nchini?

 

DK. SLAA: Ni kweli nimemaliza masomo yangu. Bado napima mazingira yaliyonifanya niondoke na familia yangu. Baada ya hapo tutaangalia uwezekano wa kurejea. Kuhusiana na siasa nadhani wanashindwa bado kuelewa niliposema nimestaafu siasa ya vyama, lakini nitakuwa tayari kupiga kelele ninapoona masilahi ya Taifa yakiumia.

Hadi sasa sijapiga kelele kwa kuwa sijaona masilahi ya Taifa yakiangamizwa, hatua mbalimbali zinazochukuliwa ni kweli zinawaumiza wasiohusika, ndio maana nilitumia katika makala mojawapo  mtego wa panya huwakamata wanaohusika na wasiohusika. Hivyo, makosa madogo mimi hayanisumbui kwa kuwa hakuna binadamu mkamilifu.

Ninatazama Katiba na sheria zetu. Kwa bahati nzuri mengi yanayotekelezwa ni utekelezaji wa vifungu vya Katiba na sheria ambazo siku zote zilikuwapo ila havikupata mtu wa kuzisimamia. JPM amejipambanua kama msimamizi makini wa Katiba na sheria zetu.

Kama watu wanaona wamenyimwa haki, basi wapiganie kwanza Katiba ya wananchi, kwa msingi wa Rasimu ya Warioba. Baada ya hapo mamlaka ya Rais yakipunguzwa wanaweza kuzungumza. Kwa leo, si tu wameitelekeza hata madai ya Katiba ya wananchi bali nayo kama ilivyo ufisadi na dawa za kulevya wameikimbia, sasa kipi kitawaingiza Ikulu 2020?

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,579FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles