Dk. Shekalaghe: Elimu ya lishe itolewe zaidi vijijini

0
881
MKUU wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dk. Seif Shekalaghe

NA SAMWEL MWANGA -MASWA

MKUU wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dk. Seif Shekalaghe ameshauri elimu kuhusu lishe itolewe hasa maeneo ya vijijini, kwani wananchi  wengi wanaoishi maeneo hayo hawana elimu ya kutosha kuhusu masuala hayo.

Dk. Shekalaghe alitoa ushauru huo wakati akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake kuhusu masuala ya lishe, baada ya kubaini elimu hiyo bado haijawafikia vizuri wananchi.

Alisema lishe ni muhimu katika ukuaji wa watoto, humfanya apate virutubisho muhimu vinavyoboresha afya ya mwili na akili, lakini wananchi walio wengi hawaipati.

 “Katika ukuaji wa mtoto, suala la lishe ni muhimu, lishe ninayoizungumza hapa ni ile lishe bora ambayo huboresha afya ya mwili na akili yake, lakini bado wananchi wengi hawana elimu hii, hasa maeneo ya vijijini,” alisema Dk. Shekalaghe.

Alisema ukosefu wa lishe huchangia watoto wengi kushindwa kukua vizuri kimwili, kiakili, hivyo kushindwa kuelewa masomo darasani sambamba na kumsababishia udumavu na kukosa nguvu za kufanya shughuli za kiuchumi ukubwani.

Dk. Shekalaghe aliitaka kamati ya lishe ya wilaya  kwenda vijijini na kutoa elimu na si kusubiri kufanya vikao na kuweka mipango mingi, lakini utekelezaji wake unakuwa hafifu.

“Sasa ni wakati wa kamati ya lishe ya wilaya kwenda maeneo ya vijijini na kutoa elimu ya lishe, si kusubiri vikao vyao na kuweka mipango mingi katika makaratasi, utekelezaji wake unakuwa  hafifu… hili halikubaliki, kila mmoja afanye kazi kulingana na majukumu yake katika kamati hiyo,” alisema Dk. Shekalaghe.

Alisema wakati mwingine umaskini unaweza kuchangia kuwapo  lishe duni kutokana na baadhi ya jamii kushindwa kumudu gharama za kununua nafaka mbalimbali kutengeneza chakula.

“Ni muhimu jamii ikawa na uelewa kuhusu lishe bora, hii itasaidia kujipanga kwa matumizi,”alisema Dk. Shekalaghe.

Alisema moja ya vipaumbele vya wilaya yake ni kuangalia namna ya kutatua changamoto za lishe, hasa maeneo ya vijijini na kuongeza bidii ya kuwaelimisha wananchi.

Dk. Shekalaghe alisema kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Chakula Duniani (WFP) iliyotolewa mwaka jana, asilimia 35 ya watoto walio chini ya miaka mitano  nchini wamedumaa kutokana na kukosa lishe bora, hali inayochangiwa na matumizi ya nafaka pekee kuandaa lishe yao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here