24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Shein: SMZ imetekeleza miradi mikubwa

Na KHAMIS SHARIF- ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuna umuhimu kwa wananchi wa Zanzibar kuendelea  kudumisha amani na utulivu uliopo nchini kwani ndio msingi wa mafanikio yanayoendelea kupatikana sasa na baadaye.

Katika risala yake ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2019 aliyoitoa kwa vyombo vya habari Ikulu jana, Dk. Shein alisema katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya mwaka 2017 – 2018 mafanikio makubwa yamepatikana ambayo kwa kiasi kikubwa yalichangiwa na kuwapo kwa hali ya amani na mshikamano.

Alisema amani na usalama uliopo nchini ni jambo muhimu linalowavutia washirika wengi wa maendeleo kuja kutembea na kuwekeza Zanzibar kutokana na kuridhika kwao na jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya SMZ.

Aidha alieleza kufurahishwa na jitihada za wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali za kujiletea maendeleo na kueleza kuwa moyo wao huo wa umoja na mshikamano umeiwezesha Zanzibar kuimarisha vizuri uchumi.

“Tukiwa tunaukaribisha mwaka mpya wa 2019, nachukua fursa hii kwa niaba ya wananchi wote wa Zanzibar kuwashukuru kwa dhati washirika wetu wa maendeleo kwa kuendelea kutuunga mkono, tunathamini mikopo, misaada na ushauri tulioupata kutoka kwao,” alisema Dk. Shein.

Aidha Dk. Shein alisema wakati unakaribishwa mwaka 2019 ni wajibu wa kila taasisi ya Serikali kujipima namna inavyoendelea kutekeleza mambo yaliyoagizwa katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015- 2020 ili kuona imekamilishwa kwa vitendo.

“Nawakumbusha viongozi wenzangu wote wa CCM tuliochaguliwa na wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, uliorudiwa mwezi Machi, 2016. Kadhalika jukumu hili wanapaswa walizingatie na wale wote niliowateua katika nyadhifa mbalimbali,” alisema Dk. Shein.

Kuhusu kasi ya utendaji wa shughuli za maendeleo kwa miaka minane ya uongozi wake, Rais Shein alisema Serikali imefikia hatua kubwa ya kuiboresha Zanzibar  kimaendeleo ili kuona nayo inajitokeza katika ramani ya dunia kiuchumi na kimaendeleo.

Alisema katika kuthibitisha ari na kasi hiyo, SMZ imetekeleza tukio moja kubwa na la kihistoria la utiaji saini mkataba wa mgawanyo wa uzalishaji wa mafuta na gesi asilia (PSA), baina ya Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia na Kampuni ya RAK GAS ya Ras Al Khaimah.

Tukio jingine la kihistoria ni kufanyika kwa Tamasha la Utalii la Kimataifa ambalo lilihudhuriwa na makampuni 150 ya utalii ya ndani na nje ya nchi ambalo lilileta mafanikio katika kuwaunganisha wafanyabiashara wa utalii wa Zanzibar na wale wa kimataifa na kuitangaza Zanzibar katika masoko duniani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles