24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Shein ataka wanunuzi nyumba kutii sheria, ramani

Na Mwandishi Wetu- Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wanunuzi wa nyumba  eneo la mradi wa nyumba za makazi Mbweni, kuheshimu sheria za ujenzi wa nyumba hizo na kuzingatia ramani.

Dk. Shein alitoa kauli hiyo katika hafla ya ufunguzi wa mradi wa nyumba za maakazi ‘ZSSF Mbweni Real estate’, iliyofanyika eneo la Mbweni nje kidogo Zanzibar..

Alisema kuna umuhimu kwa wanunuzi wa nyumba hizo kuheshimu sheria za ujenzi unaozingatia ramani halisi na hivyo kuepuka hatua zozozte za kuzifanyia mabadiliko ya muundo  au kuzipaka rangi, kinyume na taratibu.

Alisema sio jambo la busara kwa wananchi wanaonunua nyumba hizo bila ya kujali ramani halisi ya ujenzi wakaanza kuzifanyia mabadilko kwa kuzingatia kuwa nyumba hizo ni za kisasa, sambamba na kusisitiza matumizi bora na  taratibu njema za kuishi , zinazoepusha ufugaji wa aina mbali mbali za mifugo.

“Tuzingatie kwamba nyumba hizi ni za kisasa, tunahitaji tuzitumie kisasa, shughuli kama zile za kutwanga, kufuga kuku na nyenginezo itabidi tuangalie uwezekano wa kuzifanya sehemu nyengine”, alisema.

Alisema nyumba hizo ni za gharama kubwa,  akaitaka ZSSF kuondokana na muhali katika ukusanyaji wa fedha ili hatimae ziweze kulipia gharama za ujenzi.

Aliwataka wanunuzi wasighafilike kulipa madeni yao ili  iweze kupata nguvu na kubuni miradi mingine ya maendeleo.

Dk. Shein alisitiza umuhimu wa wakazi wa nyumba hizo kuendeleza silka na tamaduni za maisha ya kizanzibari kwa kuishi kwa ujirani na mashirkiano.

Alisema ujenzi wa nyumba hizo ni mfano mzuri wa namna Serikali inavyotekeleza dhamira ya matumizi bora ya ardhi iliopo, pamoja na utekelezaji wa vitendo wa azma ya muasisi wa mapinduzi matukufu ya ya Zanzibar ya 1964, marehemu Abeid Amani Karume katika kuwapatia wananchi makaazi bora, ingawaje wametumia fedha zao.

Alisema marehemu Karume, alianza na ujenzi wa nyumba za kisasa katika maeneo mbali mbali  Unguja na Pemba, ikiwemo Kikwajuni, Kilimani, Michenzani, Gamba, Makunduchi na Bambi (kwa Unguja), pamoja na Chakechake, Mkoani, Kengeja  na Wete kisiwani Pemba,  kwa kutambua kuwa makaazi bora ni miongoni mwa mahitaji ya msingi katika maisha ya binadamu.

Alisema Serikali ya awamu ya saba, kama zilivyo awamu zilizotangulia, zimekuwa zikitekeleza juhudi za kuimarisha makaazi ya wananchi, ikiwemo eneo hilo la Mbweni alilosema lina historia kubwa katika nchi. 

Alitoa shukurani kwa shirika kwa kufanikisha ujenzi huo na kubainisha matumaini yake kuwa hatua ya kuwekeza miradi ya namna hiyo itasukuma mbele maendeleo ya nchi kwa kuinufaisha jamii pamoja na kuleta haiba nzuri ya miji.

Alisema maendeleo ya nchi yoyote ile huonekana kutokana na ujenzi wa majengo na kusema ujenzi wa majengo ya kisasa katika maeneo mbali mbali ya nchi yanatoa  taswira ya maendeleo hayo.

Alilitaka shirika kuhamasiha upandaji ya miti ya vivuli katika eneo hilo, kuharakisha ujenzi wa majengo yaliobaki katika mradi huo pamoja na kuvutia wafanyabiashara  ili kuanzisha miradi mbali mbali ya utoaji huduma, kama vile kumbi za mikutano na ujenzi wa skuli.

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa alitoa shukrani kwa Dk. Shein  kwa kuitia moyo ZSSF na kufanikisha ujenzi hu na kulifanya eneo hilo kubadilika na kuwa mji mdogo.

Alitowa wito kwa sekta binafsi kuwekeza katika nyanja tofauti za utoaji wa huduma ikiwemo ujenzi wa maduka ili kuwaondolea usumbufu wakaazi wa eneo hilo kufuata huduma hizo masafa ya mbali.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Mipango. Khamis Mussa Omar, alisema mradi wa Nyumba za Makaazi eneo la Mbweni, unaohusisha majengo 15 na vyumba 210, unafanyika kupitia  Kampuni ya Kizalendo ya ‘Dezo Civil Contractors’ na pale utakapokamilika utagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 35.

Aliipongeza Serikali kwa kuipatia ZSSF eneo la ziada kwa ajili ya uendelezaji wa miradi yake pamoja na kuupongeza Uongozi uliopita wa taasisi hiyo kwa kuasisi kazi za uwekezaji na uendelezaji wa eneo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles