27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 30, 2021

Dk. Shein apongeza usalama Zanzibar

Na MWANDISHI WETU-ZANZIBARRAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amezipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na idara za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kuhakikisha Zanzibar inaendelea kuwa salama.

Dk. Shein aliyasema hayo jana wakati alipokutana na ujumbe wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ulioongozwa na Waziri Kangi Lugola, uliofika Ikulu mjini Unguja kujitambulisha.

Katika msafara huo, viongozi wengine waliofutana na Waziri Lugola ni Katibu Mkuu wa Wizara Meja Jenerali Jacob Gideon Kingu na Naibu Katibu Mkuu, Kailima Ramadhan.

Akizungumza na viongozi hao, Dk. Shein alisema Zanzibar iko salama hali ambayo imewezesha wananchi wake waendelee kuishi kwa amani na utulivu mkubwa.

Dk. Shein alisema hatua hiyo inatokana na juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na vikosi vyote vya idara zilizomo katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi likiwemo Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Idara ya Vitambulisho vya Taifa.

Alisema kupungua kwa vitendo vya uhalifu kwa asilimia 34 pamoja na makosa madogo kwa asilimia 57 kwa kipindi cha Januari hadi Oktoba mwaka huu, kumeonesha wazi kuwa mafanikio makubwa yanaendelea kupatikana katika kudumisha amani, utulivu na usalama Zanzibar.

Dk. Shein alisema kazi imefanywa vizuri sana hadi kufikia hatua hiyo ya mafanikio na kueleza imani yake kubwa aliyonayo kutokana na uongozi wa wizara hiyo ambao umeanza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Alisema viongozi hao wameingia na rekodi nzuri hatua ambayo imewezesha kuendelea kuimarika kwa hali ya utulivu, amani na usalama kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar.

Alisisitiza haja kwa uongozi wa wizara hiyo kuzitumia vyema idara zake katika kutekeleza majukumu yao kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili malengo ya waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaweze kufikiwa.

Awali Waziri Lugola alimweleza Dk. Shein mikakati maalumu iliyowekwa na wizara yake katika kuhakikisha ulinzi, amani na usalama vinakuwa vya kudumu hapa Zanzibar.

Alisema kwa kipindi cha muda wa kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu matukio ya uhalifu Zanzibar yamepungua kwa asilimia 34 na makosa madogo kwa asilimia 57 ukiwemo udhibiti wa dawa za kulevya.

Waziri Lugola alitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanaendelea kuishi kwa amani, utulivu na usalama mkubwa na kumuhakikishia vikosi vyake vya ulinzi vinasimama imara ili dira ya Zanzibar ya kudumisha amani iweze kufikiwa.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,464FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles