30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

DK. SHEIN AISIFU NMB UKUZAJI UCHUMI ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu-ZANZIBAR


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema azma ya Benki ya NMB ya kuendelea kuziunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo katika jamii, zitasaidia kuimarisha uchumi na kuleta tija kwa wananchi.

Dk. Shein aliyasema hayo juzi alipofanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa  Benki ya NMB nchini, Ineke Bussemaker, alipofika Ikulu ya Zanzibar.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema Benki ya NMB imekuwa na mchango mkubwa katika kuzisaidia sekta za maendeleo hapa nchini zikiwemo sekta ya afya, elimu na nyenginezo, hatua ambayo ni muhimu katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Dk. Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo lengo ni kuwanufaisha wananchi pamoja na kukuza uchumi na kueleza mikakati ya kuanzisha Mradi wa Huduma ya Afya kwa njia ya kimtandao e-Health.

Kutokana na hali hiyo, rais huyo wa Zanzibar aliipongeza benki hiyo kwa kuanzisha programu mbalimbali za kuwasaidia wakulima wakiwemo wa zao la karafuu hapa nchini na kueleza lengo la Serikali ni kuona zao la karafuu linaimarika na ndio maana imekuwa ikichukua juhudi za makusudi ili kuhakikisha zao hilo linapata sifa kimataifa.

“Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na NMB ni pamoja na kuwasaidia wakulima wa karafuu, kuongeza uzalishaji wa miche, kuongeza bei ya zao hilo kwa wakulima sambamba na kuanzishwa kwa mpango wa kuzipa utambulisho maalumu (Branding), karafuu na bidhaa za viungo vinavyozalishwa hapa Zanzibar.

“Pia ninapenda kukueleza kwamba zipo juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na changamoto ya ajira kwa vijana, ikiwa ni pamoja na lengo la Serikali la kuanzisha uvuvi wa bahari kuu,” alisema Dk. Shein.

Alisema miongoni mwa maeneo ya kuanzia katika changamoto hiyo ni katika sekta ya uvuvi hasa ikizingatiwa kuwa visiwa vya Zanzibar vimezungukwa na bahari, hivyo alimueleza Mkurugenzi huyo umuhimu kwa Benki yake kuisaidia sekta hiyo ili wavuvi waweze kuvua katika bahari kuu pamoja na kutumia vifaa vya kisasa.

Pamoja na hali hiyo, Dk. Shein alimhakikishia Mkurugenzi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Benki hiyo katika kuimarisha sekta za maendeleo na kukuza uchumi wa nchi na wananchi wake.

Kwa upande wake, Ineke alipongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuimarisha miradi ya maendeleo katika jamii na kuahidi kuendelea kuunga mkono.

Alisema Benki yake imekuwa ikisaidia katika kuimarisha miradi mbalimbali katika jamii ikiwemo miradi ya elimu, kilimo, afya na mengineyo na kuahidi kuiendeleza kwa lengo la kuinua kipato cha mwananchi hapa Zanzibar.

“Benki ya NMB imeweza kusaidia miradi kadhaa ikiwemo miradi ya elimu kwa kusaidia madawati, NMB inaunga mkono juhudi za elimu na hivyo tumepanga kukabidhi kompyuta 50 kwa skuli za Zanzibar,” alisema Ineke.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles