26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

DK. SHEIN AFICHUA SIRI MAZUNGUMZO NA MAALIM SEIF

Maalim Seif Sharif Hamad na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein
Maalim Seif Sharif Hamad na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

KWA mara ya kwanza tangu mazungumzo kati ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kuvunjika, rais huyo amezungumzia kilichotawala na siri ya kukwama kwake.

Maalim Seif alijiondoa kwenye mazungumzo hayo ya maridhiano baada ya kufanyika kwa takribani vikao tisa, huku wajumbe wake wakiwa pamoja na marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Dk. Salmin Amour Juma, Amani Abeid Karume na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Akizungumza jana mjini Unguja wakati wa mahojiano maalumu na mwandishi wa habari mkongwe nchini, Tido Mhando, Dk. Shein alisema mazungumzo hayo yalianza vizuri, lakini yalikuja kukwama kwa hoja moja.

“Mazungumzo yalianza kwa hali nzuri sana, kuna mambo ambayo tulikubaliana, alafu hili la uchaguzi nikasema tume ikitangaza kuwa turudie mimi na chama changu tutakubali, lakini yeye akakataa,” alisema Dk. Shein.

Alisema baada ya hali hiyo, ndipo Maalim Seif alipokatisha mazungumzo hayo na kusafiri kwenda Dar es Salaam kuzungumza na vyombo vya habari.

Alipoulizwa juu ya kikao cha maridhiano kuwa na wajumbe sita wa CCM kunaweza kutafisiriwa kwamba chama tawala kilikuwa kinapendelewa kwenye mazungumzo hayo, Dk. Shein alisema jambo hilo si sawa kwa sababu kufanyika kwake ni makubaliano ya pande mbili.

Akizungumzia ziara za Maalim Seif nje ya nchi kama zinatia doa Zanzibar na kuwatisha watawala juu ya mustakabali wa visiwa hivyo, alisema jambo hilo si kweli kwa sababu uchaguzi wa marudio ulifanywa kwa mujibu wa sheria na katiba ya visiwa hivyo, hivyo hakuna mahakama yoyote duniani inayoweza kuubatilisha.

Alisema mizozo baada ya uchaguzi ndani ya visiwa hivyo ni suala lililodumu kwa muda kabla kufanyika kwa mapinduzi na si jambo geni.

Rais huyo wa Zanzibar, alisema kuwa Serikali yake haikuingilia uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC),  ya kufuta wala kutangaza marudio ya uchaguzi huo kwani ni jambo ambalo lipo ndani ya mamlaka yao kwa mujibu wa sheria.

“Serikali kazi yake inatoa fedha za kuandaa uchaguzi tu,” alisema Dk. Shein.

Katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi mwaka jana, ZEC ilimtangaza Dk. Shein kuwa mshindi kwa kupata kura 299,982 kati ya 328,327 ambazo ni sawa na asilimia 91.4.

Akizungumzia kuhusu Muungano, alisema umekuwa imara na baadhi ya watu wanaoupinga ni wale waliokuwa wapinzani kabla ya Muungano huo.

Kutokana na hali hiyo, alisema watu hao katika siku za hivi karibuni waliibuka na hoja ya mafuta visiwani humo jambo ambalo tayari limeshatatuliwa kwa kuundwa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 na suala hilo si la Muungano.

Kuhusu suala la Katiba Mpya, alisema alishalianza na Rais mstaafu Jakaya Kikwete na sasa linasubiri kupigiwa kura ya maoni.

Alisema haoni kama kuna sababu ya kufanyiwa marekebisho yoyote yale ila isubiriwe mchakato wa kupiga kura ya maoni kwa sababu kwenye hatua zote ilishapita hadi ikapitishwa na Bunge Maalumu la Katiba.

Akizungumzia namna yake ya kufanya kazi kwa upole, alisema yeye asili yake ni kufanya kazi badala ya kuzungumza sana ingawa akiona mtu anafanya mambo yasiyofaa hasiti kumshughulikia.

Alipoulizwa juu ya hulka yake ya upole na kauli ya Rais Dk. John Magufuli aliyemtaka kuwa mkali kidogo, alisema: “Sikusema sana, napenda kufanya kazi zaidi, muulize Mkapa (Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa), Kikwete (Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete), mimi sifa yangu napenda kupima mambo, sipendi papara,” alisema Dk. Shein.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles