23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Osati: Haikuwa kazi rahisi kuufikia udatkari, kuwania urais  

Nataka taaluma hii iheshimike

                           Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

WASWAHILI wana msemo usemao ‘Nyota njema huonekana asubuhi’ akiwa amebakiza siku chache kuapishwa rasmi kuwa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Elisha Osati (35), ametunukiwa tuzo huko Ujerumani.

Dk. Osati atapokea kijiti hicho cha uongozi kutoka kwa rais anayemaliza muda wake, Dk. Obadia Nyogole, katika hafla itakayofanyika mkoani Dodoma kwenye mkutano mkuu wa 50 wa MAT.

Dk. Osati hivi sasa anasoma ubingwa wa magonjwa ya ndani katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), anatarajia kuhitimu hivi karibuni.

MTANZANIA lilifanikiwa kuzungumza naye Oktoba 10, mwaka huu saa chache kabla ya ‘kukwea pipa’ kuelekea Ujerumani kupokea tuzo yake hiyo.

“Tuzo hiyo ni ya masuala ya uongozi katika sekta ya afya ambayo hutolewa na Shirika la Inter-Academy Partnership (IAP) kwa madaktari waliopo chini ya umri wa miaka 40 waliofanya vizuri kiuongozi katika sekta ya afya.

“IAP linafanya kazi na mashirika mengine yaliyopo kila nchi duniani, hapa nyumbani wanashirikiana na Tanzania Academy of Science iliyo chini ya Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (Costech), ndiyo waliowasilisha jina langu huko,” anasema.

Anasema walipowasilisha walimjulisha na kumtaka awasilishe vyeti vyake vya kitaaluma na wasifu wake na hatimaye akateuliwa kupewa tuzo hiyo.

“Mchakato ulikuwa ni wa kidunia, walihitaji vijana 24, kati ya hao vijana watatu pekee tunatoka Bara la Afrika, sijui walizingatia vigezo gani lakini binafsi nimekuwa kiongozi kwa muda mrefu katika fani hii,” anasema.

 Si safari nyepesi

Dk. Elisha anasema safari yake ya maisha, masomo hadi kufikia hatua hiyo haikuwa rahisi.

“Ni mtoto wa tatu (wa mwisho) kuzaliwa katika familia ya Michael Osati na Hellen Nyahongo, miaka 35 iliyopita. Nilizaliwa Wilaya ya Rorya, baba alikuwa mkulima, alifariki mwaka 2001.

“Mama yangu wakati huo alikuwa mwalimu katika Shule ya Sekondari Dar es Salaam sasa ni Mhasibu katika Manispaa ya Ilala, nimeoana na Dk. Martha Nkiya tuna watoto wawili Ethan na Michelle,” anasema.

“Nimekuwa kiongozi tangu Shule ya Msingi Mbagala Kuu nikiwa kiongozi wa darasa na kiranja wa usafi, nilihitimu 1999, Shule ya Sekondari Azania nikiwa msimamizi wa midahalo (Debate Society of Azania).

“Azania kuna gazeti la shule, nikateuliwa kuwa Mhariri, kisha katibu na baadae mkurugenzi wa gazeti hilo, keptein wa timu ya shule pia Mwenyekiti Msaidizi wa Vijana wa Katoliki (TYCS) Azania na Jangwani (Aza-Jangwa), nilihitimu 2003.

“Mwaka 2006 nilihitimu kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Same, nikiwa shuleni niliteuliwa pia kuwa kepteini wa timu ya shule, kiranja wa taaluma na Katibu wa Vijana wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Same,” anasema.

Dk. Elisha anasema alijiunga na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Shirikishi (Muhas) kusoma Shahada ya kwanza ya udaktari (MD) 2011.

“Baadae nikawa kiongozi wa wanafunzi waliopo mafunzo kwa vitendo nchi nzima na kepteini wa timu ya chuo hapa Muhas,” anasema.

 Misukosuko

Anasema katika kipindi hicho ndipo walikumbana na mgomo wa madaktari wakati huo kiongozi wa MAT akiwa Dk. Stephen Ulimboka.

“Nilikuwa mafunzo kazini katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Temeke, tulikuwa tunajua tunachokipigania, maslahi bora kazini, ‘tulisukwa-sukwa’, nikawa miongoni mwa waliofukuzwa.

“Tukarudishwa ikiwa tumebakiza mwezi mmoja kuhitimu chuo, mwaka 2012 nikapata fursa kupitia mradi wa sickle cell nikafanya kazi na 2013/14 nikarudi chuoni kujiendeleza,” anasema.

Anasema akiwa chuoni hapo aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Tamsa na waliteuliwa wawili kwenda nchini Marekani kushiriki mafunzo.

“Tulipata nafasi hiyo kufuatia tafiti tulizokuwa tumezifanya chuoni, waliangalia nani aliwasilisha vizuri utafiti wake, tukapewa tuzo na Chuo cha Dartmouth Medical School huko Marekani, tulijifunza mambo mengi hasa kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” anasema.

Rais Mteule wa MAT, Dk. Elisha Osati akiwa na Rais wa Chuo cha New York Academy of Medicine (USA), Jo Ivey Boufford

Urais wa MAT

“Kulingana na Katiba yetu, makamu wa rais, ndiye anakuwa rais mteule, wakati aliyepo madarakani anapomaliza muda wake, ndipo makamu anaapishwa rasmi kuwa rais,” anasema.

Anaongeza: “MAT ni chama cha kitaaluma, kauli mbiu yetu inasema ‘Afya na Weledi’ tunataka kuleta mabadiliko na maendeleo katika sekta ya afya kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma, tunataka sekta ya afya iheshimike na isonge mbele.

Anasema ili kujidhatiti wameanza kujenga ofisi kuu huko Mbweni watatoa huduma na mafunzo endelevu kwa kujumuisha pia taaluma zingine katika fani hiyo.

 Maslahi kazini

“Ni kweli lengo ni kusimamia weledi wa kitaaluma, hiki ni chama cha kitaaluma lakini hatuwezi kuacha nyuma maslahi ya wana taaluma, hivyo tunasimamia hilo.

“Watu wapate maslahi mazuri kazini, maslahi mazuri yanajumuisha pia ubora wa mazingira ya kazi, upatikanaji wa uhakika wa dawa, vifaa tiba na posho zote wanazostahili kupewa na motisha ili kuongeza ari ya utendaji kazi.

“Kipindi kile cha mgomo ni kwa sababu hakukuwa na uhusiano mzuri kati yetu na serikali, lakini sasa uhusiano ni mzuri na tupo karibu zaidi na serikali, tunashirikiana nao kwa mambo mengi kupitia wizara,” anasema.

 Kuanzisha viwanda

“Tunataka chama kiwe na uwezo wa kujitegemea na kujitawala, tuwe chachu ya maendeleo ya viwanda,” anasema.

Anasema katika hilo wamedhamiria na wamejipanga kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini.

“Tayari madaktari wamejiunga kuanzisha viwanda na hii ni mada kuu ambayo tutaijadili katika mkutano mkuu, awamu hii fursa zipo tushindwe wenyewe.

“Tutachambua kwa kina changamoto zilizopo na jinsi gani tutazikabili, tunatarajia mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,” anasema.

Anaongeza: “Kimsingi, madaktari watarajie kuona mambo mazuri, tunataka tufanye kazi, tukianzisha viwanda maana yake tutaweza kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wakati.

 Wito kwa jamii

“Nawasihi wananchi na wanataaluma kwa ujumla waendelee kutuamini, hatutawaangusha,” anasisitiza.

Anasema: “Lakini lazima nao wajitume katika maeneo yao ya kazi hasa vijana…nimeeleza awali kwamba safari yangu haikuwa rahisi, nimelelewa na mama pekee baada ya baba kufariki.

“Nilipata shida mno wakati nasoma, hali ilikuwa ngumu kifamilia, lakini sikukata tamaa, nilisoma kwa bidii, Mwenyezi Mungu aliniwezesha na leo najivunia.

“Hivyo, sipendi na sifurahishwi na watu ambao huchukulia hali zao (ugumu wa maisha/umaskini) kama kisingizio kwamba hawawezi kufanya jambo lolote, kusonga mbele kimaisha.

“Si kweli… nilichojifunza, ukimtanguliza Mwenyezi Mungu mbele na ukiweka juhudi katika jambo lolote unalofanya, unafanikiwa… kila hatua ukiweka nguvu unasonga mbele, wasikate tamaa,” anatoa rai.

Anaongeza: “Wafanye kazi si kwa kuiga kwa sababu fulani amefanya na si kwa lengo la kujionesha kwamba wakina fulani wanione… mimi nimefanya kwa moyo, kwa bidii bila kujionesha na wala sikujua kuna watu wananiona na wanafuatilia mwenendo wangu.

“Wakaridhika, wakaniteua jina na nikachaguliwa miongoni mwa vijana wengi duniani kupewa tuzo hiyo ambayo imenifungulia milango mingi ya mafanikio.

“Pamoja na tuzo hiyo, nimepata fursa ya kujifunza zaidi masuala ya uongozi, mafunzo ambayo nina imani yatanisaidia kuimarika kiuongozi.

“Aidha, nimeteuliwa miongoni mwa jopo la wawasilisha mada tatu katika mkutano wa kidunia wa masuala ya afya (World Health Summit) na katika mikutano mingine miwili ukiwamo wa Germany & Africa Delegate, kila kitu kinawezekana,” anasisitiza Dk. Osati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles