31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Ndumbaro: Tutahimiza mabadiliko ya sheria bungeni

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro ameahidi kuhimiza wabunge wengine bungeni kushiriki kikamilifu katika kusaidia Tanzania kupata sheria nzuri za habari, kwani zitawezesha kukuza haki ya kupata habari, uhuru wa vyombo vya habari na haki ya watu kutoa maoni itakayozalisha maendeleo ya haraka kwa nchi.

Ahadi hiyo imeitoa hivi karibuni alipokutana na uongozi wa TEF na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) jijini Arusha ambapo amesema kuwa kubadilika kwa sheria kutachochea uhuru wa habari nchini.

“Binafsi niahidi hapa kwamba mimi na wabunge wengine tutashiriki kikamilifu katika kusaidia Tanzania kupata sheria nzuri za habari, kwani sheria nzuri za habari zitawezesha kukuza haki ya kupata habari, uhuru wa vyombo vya habari na haki ya watu kutoa maoni itakayozalisha maendeleo ya haraka kwa nchi yetu Tanzania,” amesema Dk. Ndumbaro.

Katika hatua nyingine Dk. Ndumbaro amemsifia Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ambaye ni mwanahabari kuwa ameonyesha nia ya kusimamia mabadiliko ya sheria hizo, hivyo ameshauri TEF na wadau kuhakikisha wanazungumza kwa karibu na Waziri huyo.

“Waziri akiwaelewa, anayo nafasi kubwa ya kulisukuma suala hili na mkabadili sheria zinazolalamikiwa ndani ya muda mfupi,” amesema.

Vyombo vya habari vipo katika mazungumzo na serikali kuomba Sheria ya Huduma za Habari, MSA 2016 irekebishwe katika vifungu vinavyofifisha Uhuru wa Vyombo vya Habari kikiwamo kifungu cha 9(a) kinachompa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) mamlaka ya kufungia vyombo vya habari bila kupitia utaratibu wa kuwasilisha malalamiko popote au pande zote mbili zilizo katika mgogoro kusikilizwa.

Jukwaa la Wahariri Tanzania na wadau, wanapendekeza mamlaka ya Mkurugenzi yafutwe na kiundwe chombo ambacho pamoja na mambo mengine kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.

Sheria nyingine zinazolalamikiwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa. Sheria hizi zina vifungu vinavyofifisha uhuru wa habari nchini hivyo zinahitaji kubadilishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles