26.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 17, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Dk. Nchimbi aonya wanaotafuta uteuzi wa bila kupingwa

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, amewaonya wanachama wanaotafuta uteuzi wa udiwani, uwakilishi na ubunge kwa njia zisizo halali, akisisitiza kuwa chama hakitasita kuwaengua wale watakaokiuka Katiba, Kanuni na maadili ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa makatibu wa matawi na kata kutoka Wilaya ya Dodoma,Dk. Nchimbi baadhi ya wanachama wanaotaka nafasi za uongozi wameanza kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha wanapitishwa bila kupingwa, jambo ambalo halikubaliki ndani ya chama.

Alieleza kuwa mabadiliko ya Katiba ya CCM yaliyofanyika chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, yalilenga kuongeza idadi ya wapiga kura katika kura za maoni ili kupata taswira pana ya maoni ya wananchi na kudhibiti mianya ya rushwa.

“Tumeanza kuona matukio ya baadhi ya wabunge na madiwani wakipitisha fomu ili watangazwe kuwa wagombea pekee. Wengine wanahamasisha vikao kutoa matamko kwamba wapitishwe bila kupingwa. Wapo wanaoandaa kumbukumbu za misiba, siku za kuzaliwa na hata sherehe za ndoa, lakini wahudhuriaji wanapewa posho na wamevaa sare za CCM ili ionekane kama mkutano wa kisiasa,” amesema.

Ameleeza kuwa CCM ina utaratibu wa kufuatilia mwenendo wa wanachama wake, na wale wote wanaoendesha kampeni za chinichini wataenguliwa mapema.

“Wengine wameanzisha NGOs kwa malengo ya kisiasa, wengine wanatumia mbinu za kuwachafua waliopo madarakani kwa sasa. Kwa wote hawa, tunasema waache mara moja. Wanapoteza muda na kutufanya tufikirie kuwaengua. Hatutavumilia mambo haya,” ameonya.

Aidha amewataka viongozi wa CCM katika ngazi zote kuhakikisha wanatenda haki kwa kusimamia Katiba na Kanuni za chama bila upendeleo.

“Mafunzo haya tunayotoa yanalenga kuwawezesha makatibu wa matawi na kata kujua dhamana yao ndani ya chama, majukumu yao na mipaka yao ya kazi. Ushindi wa CCM unategemea uimara wa mfumo wake, imani ya wanachama kwa chama, pamoja na utendaji wa Serikali yake chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
595,000SubscribersSubscribe

Latest Articles