26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 26, 2023

Contact us: [email protected]

DK. NCHIMBI AOMBWA RADHI

dk-emmanuel-nchimbi

Na AGATHA CHARLES

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), James Mwakibinga, amemwomba radhi Balozi mteule Dk. Emmanuel Nchimbi, kutokana na kumtuhumu kujimilikisha sehemu (floor) nzima katika jengo la Umoja wa Vijana (UVCCM) na kuuza kinyemela viwanja 200 vya umoja huo vilivyoko Temeke, Dar es Salaam.

Mwakibinga aliomba radhi Dar es Salaam jana mbele ya Wakili Mwandamizi wa Kampuni ya Uwakili ya FK Law Chambers, Sylivanus Mayenga, katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Katika mkutano huo, Mwakibinga alisema baada ya kutoa tuhuma hizo alizozipata kupitia vyanzo visivyo rasmi, alifanya uchunguzi ili kujiridhisha na kugundua alidanganywa na hazikuwa za kweli.

“Suala la kumgusa Dk. Nchimbi ni ajali ya kisiasa, hivyo kuomba radhi ni kitendo cha uungwana. Nachukua fursa hii kumwomba radhi Dk. Nchimbi ambaye ni mlezi na kiongozi wa mfano kwa sababu siasa ni mapito. Nimegundua tuhuma hizo hazina ukweli wowote,” alisema Mwakibinga.

Akijibu swali kwamba iwapo madai hayo aliyatoa kutokana na kushawishiwa na mtu au kundi fulani, Mwakibinga, alisema huo ulikuwa ni utashi wake kutokana na hulka yake ya kuhoji mambo.

“Sikutumwa na mtu wala kundi, ilikuwa ni utashi wangu na weledi. Baada ya kutakiwa na mawakili wake kuthibitisha madai hayo nilijiridhisha pia kuwa UVCCM haijawahi kumiliki viwanja Temeke, naahidi kuwa nitakuwa nafanya utafiti kabla ya kuongea jambo lolote. Napongeza pia CCM inafuatilia na kukagua miradi ya vijana na kusoma mapato na matumizi,” alisema.

Mwakibinga alisema pamoja na kuomba huko radhi hatafumba mdomo kuhusu uzalendo ili CCM ijiendeshe kiuchumi pasipo kutegemea fedha za wafanyabiashara.

Naye Mayenga alisema baada ya mdaiwa huyo kuomba radhi atafanya mawasiliano na mteja wao (Dk. Nchimbi), ili kuona namna wanavyoweza kufuta kesi ya madai namba 300 ya 2016 iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyodai fidia ya Sh bilioni moja.

“Nitazungumza na mteja wetu (Dk. Nchimbi) ili shauri namba 300 la madai mwaka 2016 Kisutu tuweze kuliondoa, tuhuma zilikuwa kubwa na madai yalikuwa fidia ya shilingi bilioni moja. Kuomba radhi ni uungwana na tunapaswa kufanya utafiti kabla ya kuzungumza ili kusaidia kuondoa migogoro na tujenge nchi,” alisema.

Mayenga alisema shauri hilo lilikuwa katika hatua ya kutajwa lakini mhusika hakuweza kujitokeza mahakamani na zaidi aliomba lizungumzwe ili liishe.

Mwakibinga alitoa tuhuma hizo dhidi ya Dk. Nchimbi Agosti 16, mwaka jana  katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Siku kadhaa baada ya mkutano huo, Dk. Nchimbi kupitia wakili wake alimpa Mwakibinga siku 14 ili kumwomba radhi kabla ya kumchukulia hatua zaidi ikiwamo kwenda mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,726FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles