24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mwidimi Ndosi: Tutaishinda Corona kwa kuchanja

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wakati aina mpya ya kirusi cha Corona (Delta) ikisambaa kwa kasi duniani wanasayansi wamesema njia pekee ya kukikabili ni kupata chanjo.

Inaelezwa kuwa kirusi hicho kina nguvu ya kuambukiza mara mbili zaidi ambapo mtu mmoja anaweza kuambikiza watu sita tofauti na kirusi cha awali ambapo mtu mmoja aliambukiza watu watatu.

Akizungumza wakati wa mkutano ulioandaliwa na Shirika la Internews Tanzania na kushirikisha wanahabari na wadau mbalimbali wa afya, Mtafiti na Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Uuguzi cha Rheumatology (University of the West of England, Bristol) Dk. Mwidimi Ndosi, amesema virusi vinapokaa kwa muda mrefu bila kudhibitiwa vina kawaida ya kujibadilisha kama ilivyotokea kwa delta.

“Chanjo ni kinga muhimu tutazuia virusi kujibadilisha kwa kudhibiti ugonjwa, kuwa na virusi kwa muda mrefu kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kujibadilisha, ambaye hajachanja anakuwa kiwanda cha kutengeneza virusi na kinavyojibadilisha ndipo kinaenea zaidi”, amesema Dk. Ndosi.

Dk. Mwidimi Ndosi.

Akizungumzia ufanisi wa chanjo zilizothibitishwa ikiwemo ya Johson& Johnson amesema ulifanyika utafiti kujua uwezekano wa kupata maambukizi kati ya watu waliopata chanjo hiyo na ambao hawakupata na kubaini imepunguza uwezekano wa kupata maambukizi kwa wale waliochanja.

Ametoa mfano wa baadhi ya nchi kama Marekani ambapo kati ya watu 1,779 waliochanjwa chanjo hiyo na kufuatiliwa baada ya wiki mbili watatu ndiyo walipata maambukizi wakati kwa wasiochanjwa 17,744 waliopata maambuki ni 128.

“Uwezekano wa maambukizi umepunguzwa zaidi ya mara nne, ufanisi halisia ni asilimia 76.7 kwenye kuzuia maambukizi, kwa Afrika Kusini imeonyesha ufanisi kwa asilimia 100”, amesema.

Aidha amesisitiza kwa waliochanja kuendelea kujikinga ili kudhibiti ugonjwa huo kwani licha ya kwamba hawataathirika lakini watakuwa chombo cha kubeba maambukizi na kuambukiza wengine.

“Ukipata chanjo endelea kujikinga kwa sababu unaweza kugusa sehemu yenye maambukizi ukampatia mtu mwingine au unaweza kuvuta hewa wewe hutaathirika lakini unakuwa chombo cha kubeba ile hewa, unaweza ukavuta hewa ukaitoa kwa mtu mwingine ambaye hana maambukizi,” amesema.

Dk. Ndosi ameishauri Serikali kuendelea kuhamasisha jamii kuchukua tahadhari na kwenda kupata chanjo ili kuzuia uwezekano wa kuzalishwa virusi vipya.

Naye Mkufunzi Mwandamizi kutoka Internews Tanzania, Alakok Mayombo, amesema vyombo vya habari vina wajibu kwa jamii na kuvishauri kuepuka kutoa taarifa potofu.

“Ukiandika habari ambayo imekaa ndivyo sivyo unahatarisha maisha ya watu, katika suala la Corona tunajua faida na hasara pale ambapo taarifa zinakuwa kinyume, taarifa sahihi zinaokoa maisha na zisipokidhi viwango zinaweza kuangamiza jamii,” amesema Mayombo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles