26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mwakyembe: wabunge Ukawa wanyimwe mshahara

Dk. Harrison MwakyembeNa Mwandishi Wetu, Dodoma

HATUA ya wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani  kususia vikao vya Bunge imechukua sura mpya, baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe  kutaka wabunge hao wasilipwe posho na mishahara yao.

Ametoa pendelezo hilo baada ya wabunge hao kutangaza mgogoro na Naibu Spika, Dk. Ackson Tulia na kususa vikao vitakavyoongozwa na kiongozi huyo wa Bunge wakisema   analiyumbisha Bunge.

Akiomba mwongozo wake bungeni jana   baada ya kipindi cha maswali na majibu, Dk. Mwakyembe alisema  wabunge hao hawapaswi kulipwa posho wala mshahara kwa mujibu wa Ibara ya 23 ya Katiba.

Akinukuu ibara hiyo alisema: “Kila mtu bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake na watu wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao watapata malipo kulingana na kazi wanazofanya.

“Naomba mwongozo wako, wabunge tunaoingia hapa bungeni kwa sekunde kadhaa na kuondoka na wengine wanabonyeza vitufe vidole vya mahudhurio na kwenda kupumzika na kuwaacha wabunge wengine wakifanya kazi kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi.

“Je mheshimiwa Spika, mbunge anayeamua kwa hiari yake kujiondoka katika sehemu yake ya kazi na kwenda kupumzika ana haki chini ya  Ibara ya 23 kulipwa posho sawasawa na wabunge wengine ambao wanaendelea na kazi?” aliuliza.

Dk. Mwakyembe pia alitaka kujua uongozi wa Bunge unafanya nini kuhusu utekelezaji wa kanuni ya 75 inayotaka wabunge waliosimamishwa kulipwa nusu posho na nusu mshahara.

Musukuma

Naye Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma (CCM), alisimama na kuomba mwongozo kuhusu jambo hilo, huku akitaka kanuni za Bunge zifanyiwe marekebisho   kuwazuia wabunge wanaofukuzwa bungeni kufanya mikutano majimboni mwao.

“Suala hili tumeuliza sana, nilianza kuliuliza mimi, jana (juzi) kauliza mh Kessy (Mbunge wa Nkasi) leo (jana) kauli mh Mwakyembe kuhusu wabunge wanaobofya na kuondoka.

“Na tumekuwa tukipewa majibu hayo hayo ‘mwongozo tutautoa baadaye, tutautoa baadaye’, sasa nilitaka kupata mwongo wako.

“Kama kiti chako kinapata kigugumizi kutoa mwongozo huu kwa nini suala hili lisiingie kwenye Kamati ya Kanuni  tukatengeneza kanuni ambazo zitawabana na wenzetu tukaweza kushirikiana nao.

“Lakini pia hata wale wabunge waliosimamishwa. Unawasimamisha bungeni, unawalipa nusu posho, unawalipa nusu mshahara na wanaendeelea kufanya mikutano ya kibunge kwenye majimbo.

“Hauoni kama hawatutendei haki, kwa nini kanuni hizi zisiwabane wakasimamishwa hadi kwenye majimbo  tukatapa heshima na adabu?” alisema.

Akijibu mwongozo huo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alisema jambo hilo limekuwa likijitokeza lakini katika mazingira tofauti tofauti na hivyo linapopokelewa linachukuliwa kama mwongozo mpya.

Kuhusu mwongozo wa Dk. Mwakyembe, Dk. Tulia hakuweza kuitolea mwongozo hoja ya kutaka wabunge wanaosaini na kuondoka bila kufanya kazi, akisema  mwongozo huo utapatiwa majibu baadaye.

Kwa siku ya tatu jana, wabunge wa kambi ya upinzani wamekuwa wakiingia bungeni na kutoka, kama sehemu ya utekelezaji wa azimio lao la kumsusa Naibu Spika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles