24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mwakyembe agonga ukuta bungeni  

Dk.-Harrison-MwakyembeNa Khamis Mkotya, Dodoma

HOJA ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe kutaka wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni wasilipwe posho na mshahara kwa  kuendelea kususa vikao vya Bunge imegonga ukuta.

Dk. Mwakyembe   aliomba mwongozo huo Juni 2, mwaka huu akitaka kujua kama ni haki kwa wabunge hao kuendelea kulipwa  wakati Ibara ya 23 ya Katiba inasema mtu atalipwa ujira kulingana na kazi anayofanya.

Alisisitiza kuwa wabunge hao  hawapaswi kulipwa kwa sababu  ni sawa na kuwalipa wabunge hewa.

Akitoa majibu ya mwongozo wake bungeni jana baada ya kipindi cha maswali na majibu, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson alisema wabunge hao wataendelea kulipwa kwa kuwa malipo yao yapo kwa mujibu wa sheria.

Naibu Spika alirejea uamuzi wa kiti uliowahi kutolewa bungeni Aprili 27, 2016 katika mwongozo kama huo ulioombwa na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM).

“Wakati akiomba mwongozo wa Spika, Mh Kessy (Ally) alieleza kitendo cha wabunge wa upinzani kuingia bungeni kusaini na kuondoka ilihali wanalipwa posho na mshahara ni sawa na watumishi hewa.

“Dk Mwakyembe katika mwongozo wake alitaka kujua kama wabunge wa upinzani wanaoingia bungeni kusaini na kuondoka wana haki ya kulipwa kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 23.

“Kutokana na uamuzi uliowahi kutolewa na Bunge hili   Aprili 27  kuhusu mwongozo wa Spika unaofanana na mwongozo wa wabunge hawa wawili  ambao uliombwa na Mh Hussein Bashe.

“Bashe  aliuliza kuhusu usahihi wa wabunge wa upinzani kulipwa posho na mshahara wakiwa hawatimizi wajibu wao.

“Katika kujibu mwongozo wa Bashe, kiti kilinukuu Ibara ya 73 ya Katiba inayosema wabunge wote wa aina yote watashika madaraka yao kwa mujibu wa Katiba hii na watalipwa mshahara, posho   na malipo mengine kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.

“Kiti kiliendelea kutoa uamuzi wake kama ifutavyo: masharti ya kazi ya mbunge yanaeleza kwamba mbunge anastahili kulipwa mshahara kila mwezi.

“Masharti hayo yamefafanua kuwa  mbunge anapohudhuria vikao vya Bunge   na kamati zake atalipwa posho kwa viwango vitakavyowekwa na Serikali kwa kuzingatia Sheria ya Fedha na kanuni zake,” alisema.

Naibu Spika alisema malipo ya mshahara kwa mbunge ni suala la  katiba na  sheria na kwamba malipo hayo hulipwa kwa kazi yake ya ubunge kama yalivyotajwa katika Ibara ya 73 ya Katiba.

Hata hivyo Dk. Tulia alisema iko haja kwa siku zijazo kuzifanyia marekebisho ya sheria zilizopo  kukabiliana na hali ya namna hiyo na kuweka utaratibu mahususi.

Tulia alisema utaratibu huo utawezesha kila mbunge kulipwa posho baada ya kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikizingatiwa kusaini mahudhurio pekee haitoshi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles