*Wafadhili wa nje kutoendelea kutoa fedha
Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
MTIKISIKO mkubwa unaweza kuikumba sekta ya afya baada ya muda wa miradi mikubwa iliyokuwa inatekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) nchini kufika mwisho.
Miradi hiyo mikubwa ni pamoja na ile ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na misaada ya ufundi katika sekta hiyo, utoaji wa elimu kwa wanazuoni, usambazaji na usimamizi wa vifaa vya tiba kwa miaka 10 iliyopita.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubsya alisema Dar es Salaam jana kuwa:
“Wadau hawa walikuwa katika miradi ambayo ilikuwa chini ya USAID katika kupambana na malaria na mfumo wa utoaji na usambazaji wa dawa za kupambana na Ukimwi kupitia mradi wake wa SCMS.
“Walikuwa wanatoa huduma hizo kwa kushirikiana na taasisi nyingine za afya nchini ikiwamo Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na Bohari ya Dawa (MSD),” alisema.
Dk. Ulisubsya alisema miradi hiyo imesaidia kuongeza idadi ya watu wanaotumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (Arv’s) kutoka watu 150,000 miaka 10 iliyopita hadi kufikia watu 800,000 hivi sasa.
“Miradi hii imesaidia pia katika kufanikisha ujenzi wa maghala makubwa na ya kisasa ambayo yamepunguza gharama za utunzaji wa dawa ambazo MSD ilikuwa inalipia kutunza kwa watu binafsi…imetuwezesha pia upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya umeme,” alisema.
Katibu Mkuu huyo aliweka wazi kuwa wadau kama hao wanapoondoka nchini baada ya muda wao wa kusimamia miradi kuisha, miradi hiyo hutetereka katika uendeshaji na hata kufa.
“Lakini ili kukabiliana na hali hiyo, serikali imejipanga kuwatumia wataalamu ambao walisaidiwa mafunzo katika ngazi mbalimbali za afya na wadau hawa wakati miradi ilipokuwa ikiendeshwa mambo yaweze kwenda sawa sawa,” alisema.
Alisema serikali pia imejipanga kupitia bajeti ya mwaka huu, kuhakikisha inafanikisha uendeshaji wa mipango mbalimbali katika sekta ya afya.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laureen Bwanakunu alisema Mamlaka hiyo imeweza kufanya miradi mikubwa ambayo ilifadhiliwa na USAID katika kipindi hicho ikiwamo ujenzi wa maghala makubwa ya kuhifadhia dawa, yenye thamani ya Sh bilioni 30.
Pigo sekta ya afya
Taarifa za kuondoka kwa wafadhili hao zinaweza kuwa pigo kubwa kwa katika sekta ya afya nchini kutokana na miradi hiyo kutegemea wafadhili wa nje kwa asilimia 90 huku Marekani ikiwa kinara wa ufadhili huo.
Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa baadhi ya miradi ambayo wafadhili waliwahi kujitoa, imedorora au imekufa.
Miradi hiyo ni pamoja na Mpango wa Taifa wa Damu Salama ambao awali ulikuwa ukifanya vizuri, lakini hivi sasa umetetereka baada ya wadau kujitoa na kuukabidhi kwa serikali.
Hivi karibuni, Meneja Mpango wa Damu Salama Kanda ya Mashariki, Dk. Aveline Mgasa alinukuliwa akisema kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa damu tangu mwaka 2014 baada ya kukosekana misaada kutoka kwa wafadhili.
Dk. Mgasa alisema hayo mbele ya Naibu Waziri wa Afya, Dk. Hamis Kigwangwala alipofanya ziara ya kushtukiza katika kitengo hicho baada ya wananchi kulalamikia kukosekana damu ya kutosha hospitalini.
“Wafadhili hao walikuwa wanawezesha mpango huu kwa kutoa fedha ambazo zilikuwa zinatumika kutafuta damu. Tuliweza kufanikisha ukusanyaji wa damu vizuri katika kipindi cha 2007 hadi 2014 walipojitoa.
Chanzo kingine kutoka Wizara ya Afya kiliieleza MTANZANIA kuwa miradi yote ya afya ikiwamo ya uzazi wa mpango na ule wa dawa za kutuliza makali ya Ukimwi (Arv’s) inategemea ufadhili kutoka Marekani.
Mradi wa ‘sickle cell’ Muhimbili
Hivi karibuni, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ilisimamisha ghafla matibabu ya bure kwa wagonjwa wa seli mundu (sickle cell) ambao walikuwa wakitibiwa kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza kupitia shirika la Welcome Trust.
Shirika hilo lilifadhili matibabu hayo kwa miaka 10 na ulikuwa ukisimamiwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) tangu mwaka 2004 na ulihitimishwa Machi, mwaka huu.
Baada ya kuisha mradi huo, Muhimbili imelazimika kuwarudisha wagonjwa wapatao 6,000 waliokuwa wakitibiwa kupitia mradi huo kwa kuwapa rufaa kwenda hospitali za wilaya ambako hata hivyo hakuna huduma ya kliniki maalumu kwa ajili yao.
MNH yaishiwa chanjo ya mbwa
Vilevile, jana gazeti hili lilipata taarifa kuwa hospitali hiyo imeishiwa chanjo ya kumkinga mtu aliyeng’atwa na mbwa ili asipatwe na kichaa cha mbwa, ‘anti-rabies’.
Hivi sasa ili mgonjwa apate chanjo hiyo analazimika kuinunua katika maduka nje ya hospitali ingawa sheria hairuhusu kuuzwa katika duka lolote la dawa.
Akizungumza na MTANZANIA jana, mwananchi mmoja, Nelly Rajab ambaye mwanawe, Erick Rajab, aling’atwa na mbwa na hivyo kuhitaji kupata chanjo hiyo, alishangazwa na dawa hiyo kutokuwapo hospitalini hapo.
“Mwanangu Erick aling’atwa na mbwa nikampeleka Hospitali ya Palestina wakanipa rufaa ya kwenda Mwananyamala na huko wakanipa rufaa ya kuja Muhimbili lakini nilipofika hapa niliambiwa dawa hakuna.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alikiri hospitali hiyo kuishiwa dawa hizo kwa mwezi mmoja sasa. Hata hivyo alisema wamekwisha kuziagiza MSD.
Mkurugenzi wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema zimepokelewa chupa 2,000 za dawa hizo kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) wiki iliyopita ambazo zimekwisha kuanza kusambazwa katika hospitali mbalimbali za serikali.
Habari hii imeandikwa na Mauli Muyenjwa, Secilia Alex na Veronica Romwald, Dar es Salaam.