24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mpango kuifikia miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 111.6 Mwanza

Na Clara Matimo, Mwanza

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango anatarajia kuikagua,  kuzindua na kuweka jiwe la msingi kwenye  miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 111 katika ziara yake  ya siku tatu Mkoani Mwanza.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 10,2022 na Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima wakati akitoa taarifa ya ziara ya Dk. Mpango mkoani humo kwa waandishi wa habari ambapo alieleza kwamba kati ya miradi hiyo imo ya afya, maji na miundombinu.

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.

Malima amesema Dk. Mpango anatarajia kuanza ziara  ya kikazi mkoani Mwanza Septemba 12 hadi 14 mwaka huu, huku akifafanua kwamba Septemba 13 atazindua miradi mitatu ambayo ni  jengo la wodi ya saratani  katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando lililogharimu zaidi ya Sh bilioni 5.6.

Jengo la mama na mtoto  lililojengwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure lenye thamani ya Sh bilioni 10.1 ambalo litaboresha huduma za afya kwa wananchi hususani akina mama na watoto pamoja na stendi ya kisasa ya mabasi na maegesho ya malori ya Nyamhongolo iliyopo Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza ambayo imegharimu Sh bilioni 26.6 itakayoongeza mapato ya halmashauri kwani inakadiriwa kukusanya Sh bilioni 2.2 kwa mwaka.

“Huduma zitakazotolewa kwenye jengo la wodi ya  saratani bugando ni matibabu kwa njia ya mionzi(radio therapy), dawa za kinyuklia(nuklear medicine), matibabu ya utoaji wa dawa (chemotherapy), huduma za kuona wagonjwa wa nje na kulaza wagonjwa wodini.

“Kukamilika kwa jengo hilo kutawapunguzia gharama wakazi wa mikoa ya kanda ya ziwa watakaopata matatizo ya saratani kufuata matibabu jijini Dar es Salaam hospitali ya ocean Road maana watayapata bugando,”amesema Malima  na kuongeza

“Nawaomba wakazi wa mkoa wetu wa Mwanza na mikoa jirani waje tuungane na Mheshimiwa Makamu wa Rais Dk. Mpango kwenye uzinduzi wa miradi hii tuunge mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika kutatua kero za wananchi na kuwasogezea huduma mbalimbali karibu,” amesema.

Kwa mujibu wa Malima Septemba 14, 2022 Dk. Mpango ataweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji Butimba kilichopo Wilaya ya Nyamagana mkoani humo unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira(Mwauwasa) unaotekelezwa kwa gharama ya Sh bilioni 69.3.

 Amesema mradi huo mkubwa ambao utazalisha lita za maji milioni 48 kwa siku hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 40 na unategemewa kukamilika Februari 2023.

“Mradi huo ukikamilika utaboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi kwa wakazi wapatao 450,000 katika jiji la Mwanza, kama nilivyosema awali  zote hizi ni jitihada za serikali katika kuhakikisha inatatua changamoto za wananchi wake kwenye sekta mbalimbali,” amesema Malima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles