ASHA BANI-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema riba za mikopo bado ziko juu kiasi kwamba watu wengi wanashindwa kukopa na baadhi kushindwa kurejesha mikopo wanayokopa.
Dk. Mpango alisema hayo jana wakati alipomwakilisha Rais Dk. John Magufuli katika mkutano wa 19 wa taasisi za fedha nchini.
Alisema angependa mkutano huo utoe mikakati ya kushusha riba ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo na kuchochea maendeleo ya uchumi.
“Aidha itafaa kongamano hili libainishe mikakati mipya ya kupunguza na kudhibiti kiasi cha mikopo chechefu katika mabenki,” alisema Dk. Mpango.
Alisema upatikanaji wa mikopo ksekta ya kilimo bado hauridhishi.
“Sekta ya kilimo ni muhimu siyo tu katika kutoa malighafi kwa ajili ya viwanda, lakini pia kama nilivyokwishasema, ndiyo chanzo kikuu cha chakula na fursa za ajira kwa Watanzania wengi, lakini pia ndiyo sekta yenye uwezo wa kupunguza umasikini na kuchangia upatikanaji wa fedha za kigeni kwa kiasi kikubwa,” alisema Dk. Mpango.
Kutokana na hali hiyo alitaka mjadala huo unaoendelea hadi leo, uangalie namna bora ya kuzifanya taasisi za fedha kuongeza mikopo ya riba nafuu kwa kilimo cha mazao, ufugaji, uvuvi na biashara husika.
Hata hivyo, alisema anaungana na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Florens Luoga, kutambua juhudi zinazofanywa na wadau kuboresha sekta ya fedha, ikiwemo kujenga kanzidata za taarifa za wateja na utoaji wa vitambulisho vya taifa.
Alitoa rai kwa mamlaka husika kuharakisha utoaji wa vitambulisho vya taifa na benki kwa upande wao kuhakikisha zinaboresha utoaji wa huduma za kifedha.
Dk. Mpango alisema Serikali inaendelea na ujenzi wa miradi ya kimkakati, ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ambayo itarahisisha usafirishaji na uchukuzi, ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya maji Mto Rufiji (2115 MW) na maboresho ya sekta ya anga.
Alisema Serikali ya awamu ya tano wakati inaingia madarakani, wastani wa makusanyo ya kodi kwa mwezi yalikuwa Sh bilioni 850, lakini sasa ni Sh trilioni 1.3.
“Hata hivyo, kwa miezi ya hivi karibuni tumekuwa tukikusanya wastani wa zaidi ya Sh trilioni 1.5 kuanzia Julai hadi Oktoba 2019 na sekta ya fedha imekuwa miongoni mwa walipakodi wazuri,” alisema.
Akizungumzia sekta isiyo rasmi, alisema bado ni kubwa na haipati fursa ya kutosha kunufaika na huduma rasmi za kifedha.
Alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kurasimisha rasilimali na biashara, ikiwa ni pamoja na utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo.
“Lengo ni kuwawezesha wajasiriamali hao kuingia kwenye mfumo rasmi ili waweze kushiriki kikamilifu katika ukuzaji uchumi.
“Natoa changamoto kwenu taasisi za fedha kuhakikisha mnatoa huduma ambazo zitawawezesha wajasiriamali hao kuingia kwenye mfumo rasmi ili waweze kushiriki katika ukuaji wa uchumi,” alisema Dk. Mpango.
Naye Profesa Luoga alisema mkutano huo unalenga pamoja na mambo mengine kuharakisha maendeleo ya sekta ya fedha nchini.
Alisema kutokana na juhudi mbalimbali za kuboresha sekta ya fedha, wameshuhudia mafanikio makubwa.
“Sekta hii imekuwa kwa wastani wa asilimia 3.1 na ikichangia katika ukuaji wa uchumi kwa wastani wa asilimia 2.6 katika kipindi cha miaka mitano inayoishia 2018.
“Taasisi za fedha zimeendelea kusambaa sehemu mbalimbali nchini na mpaka sasa kuna benki za biashara na taasisi za fedha 61 zenye matawi 838 nchini.
“Na Benki Kuu imekuwa ikisisitiza upatikanaji wa huduma karibu na wananchi ambapo jumla ya mawakala 22,481 wa benki wanatoa huduma moja kwa moja kwa wananchi,” alisema Profesa Luoga.