Clara Matimo, Mwanza
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, amemuagiza Naibu Waziri wa OR- TAMISEMI David Silinde kukagua mwenendo wa uendeshaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe iliyopo Mkoani Mwanza kutokana na uwepo wa malalamiko mengi ya ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Pia amemuagiza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuchunguza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe Nansio ambayo serikali imepeleka Sh bilioni 3, lakini ujenzi unasuasua.
Dk. Mpango ametoa agizo hilo Novemba 25, 2022 wilayani humo wakati akihutubia wananchi wa Wilaya hiyo kwenye viwanja vya Getrude vilivyopo Nansio Ukerewe.
“Ujenzi wa mradi wa Hospitali ya wilaya unadaiwa kuhujumiwa naagiza baada ya uchunguzi hatua kali zichukuliwe kwa wote watakaobainika kuhusika katika uhujumu wa mradi huo, wakiwashinda waleteni kwangu mtaona nitakachowafanya,”aliagiza Dk. Mpango.
Pia Dk. Mpango ameitaka Wizara ya Maji kusimamia kwa ukaribu mradi mkubwa wa maji Kaziranganda wenye thamani ya Sh bilioni 7 na mingine 11 inayotekelezwa na serikali ili ikamilike kwa ufanisi na mapema iwasaidie wanachi kuondokana na changamoto ya maji.
Naibu waziri wa Wizara ya Maji, Maryprisca Mahundi amesema wilaya ya Ukerewe inapata huduma ya maji kwa asilimia 56 ya mahitaji ya wananchi wake na miradi 11 inaendelea kutekelezwa yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 16 ambayo ikimakilika wilaya hiyo itakuwa na ongezeko la asilimia 26 ya upatikana wa huduma ya maji na lengo la serikali ni kufikia asilimia 85 ifikapo mwaka 2024 kwa kuwa ndiyo ahadi ya ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Meja Jenerali Suleiman Mzee ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mara amemuahidi Dk. Mapngo kwamba uongozi wa mkoa huo utayafanyia kazi maagizo yote aliyoyatoa kwa viongozi mkoani humo.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Reuben Sixbeth, ameiagiza Kamati ya siasa ya Wilaya ya Ukerewe kufuatilia kwa kina miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa na serikali wilayani humo ambayo haijakamilika ili ikamilike kwa wakati uliopangwa ikiwa na thamani halisi ya fedha zilizotumika.
“Katika wilaya hii CCM imetekeleza ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025 kwa asilimia 60 sisi ambao ndiyo wenye duka hatutakuwa tayari kuharibiwa na wauza duka letu kwa tunawahudumia hivyo nakuahidi Mheshimiwa Makamu wa Rais Dk. Mpango tutafuatilia kila mara na sasa naiagiza kamati ya siasa ya wilaya kufuatilia kwa kina miradi y maji ambayo inasuasua pamoja na ujenzi wa Hospitali ya wilaya ambayo pamoja na uwepo wa fedha bado haiendi vema,”amesema Sixbeth.
Mbunge wa Jimbo la Ukerewe Joseph Mkundi ameishukuru Serikali kwa kuwaletea wananchi wa jimbo hilo fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya barabara, afya, elimu, umeme na maji.
“Kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Ukerewe napenda kuishukuru sana serikali kwa kutupatia pampu mbili mpya kwenye mradi mkubwa wa maji ambao utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi,”amesema Mkundi.
Awali kabla ya kuhutubia wananchi Dk. Mpango alikagua na kufungua mradi wa Shule ya Sekondari ya Ukerewe wenye thamani ya Sh bilioni 1.1 kutoka Serikali kuu ambapo aliwapongeza viongozi wa Wilaya hiyo kwa utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya elimu na akawataka kukamilisha ujenzi wa maabara ya fizikia.
Pia alikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Igalla wilayani humo kilichogharimu Sh milioni 492,370,000 kati ya fedha hizo Sh milioni 490,000,000 mapato ya ndani na Sh milioni 2, 370,000 mchango wa wananchi kinachotarajia kuwanufaisha wananchi zaidi ya 17,000 ambapo aliagiza ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 2023 kuanza kutolewa kwa huduma za Afya kwenye Kituo hicho ili wananchi wa eneo hilo wapate huduma muhimu ya afya jirani na makazi yao.
Akiwa mkoani Mwanza kote alikohutubia wananchi na kufanya ziara yake ya kikazi Dk. Mapango aliwasisitiza kutunza mazingira, vyanzo vya maji,wapande miti, waache kutupa takataka hovyo kwa faida yao na vizazi vya sasa na vijavyo pia waendelee kudumisha amani na mshikamano baina ya watanzania wote.
Vilevile aliwaomba viongozi wa dini kuisaidia serikali kukemea mimba za utotoni kwani watoto wa kike wanapojifungua kabla ya umri wanakosa nafasi ya kuendelea na masomo pia wanapata madhara mbalimbali ya kiafya ikiwemo ugonjwa wa fistula.
Dk. Mpango alikuwa Mkoani Mwanza kwa ziara ya siku nne ya kikazi tangu Novemba 22,2022 amehitimisha leo Novemba 25,2022 katika Wilaya ya Ukerewe.