Dk. Migiro: Hata Uingereza tunapiga nyungu

0
975

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

BALOZI wa Tanzania nchini Uingereza, Dk. Asha-Rose Migiro, amesema katika kukabiliana na virusi vya corona, hata huko waliko nako wanapiga nyungu (kujifukiza) kama kawaida maana kila mtu anatafuta namna ya kujiokoa.

Hayo aliyasema jana na kufafanua kwamba licha ya yeye na Watanzania wengine kuwepo Uingereza, wanatambua nyungu ni kitu cha asili na wanapiga nyungu.

“Unajua kila mtu anatafuta njia mbalimbali za kujiokoa,” alisema Dk. Migiro.

Akifafanua zaidi wakati anahojiwa na kipindi cha 360 kilichorushwa jana na Clouds Media, Dk. Migiro alisema pia anatambua jitihada mbalimbali ambazo zinafanywa na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania katika kutafuta dawa ya kukabiliana na corona.

“Kuna hatua ambazo zinaendelea kwa nchi za Afrika, kama ambavyo tunafahamu kwa sasa corona haina dawa wa kinga, hivyo kila nchi inajaribu kuangalia namna ya kusaidia wananchi kwenye janga hili. 

“Hata dawa ya Madagascar  napongeza Rais Dk.John Magufuli alivyoamua kutuma ndege kwa ajili ya kuifuata.

“Tunafahamu mataifa yote yanahaha kutafuta dawa na hadi sasa hakuna dawa ambayo imethibitika kisayansi kuwa inatibu corona, hivyo dawa ambayo itapatikana kwa sasa basi hiyo hiyo itatumika, maana hata unapozuia watu wasinywe, kuna tiba ipi nyingine mbadala ambayo unampa atumie. Hivyo dawa ambayo imetolewa na Madagascar kwa Tanzania ni hatua nzuri.

“Na nimeona kupitia mitandao kwetu hapo nyumbani Tanzania kuna jitihada ambazo zinafanyika kupata dawa, na nimeona kuna dawa imeonekana kuwa na uwezo wa kutibu corona. Kwa kweli ni hatua nzuri kwa nchi za Afrika katika kupambana na ugonjwa huu,” alisema Dk. Migiro.

Kuhusu uwepo wa Watanzania nchini Uingereza wenye kupatwa na maambukizi ya corona, Dk. Migiro alisema kuwa kwa taarifa ambazo wanazo idadi ya waliopatwa na maambukizi ni Watanzania kati ya 15 hadi 20.

“Ukweli wapo Watanzania ambao walipatwa na maambukizi ya corona hapa Uingereza, lakini wengi wanaendelea vizuri tu na afya zao zimeendelea kuwa imara,” alisema Dk. Migiro. 

Alisema kuwa kwa sasa Uingereza ndio inayoongoza kwa Bara la Ulaya kwa kuwa na idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha kutokana na corona.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here