30.4 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Kuruswa azindua Mfumo wa Ushirikishwaji wa Watanzania Sekta ya Madini

*Watanzania waendelea kunufaika Sekta ya Madini, ajira 15,341 zamwagwa, *Manunuzi ya ndani ya nchi yafikia Dola za Marekani bilioni 2.22

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amezindua rasmi mfumo wa ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content) na wa utoaji wa huduma kwenye jamii unaofanywa na migodi ya madini (CSR)

Dkt. Kiruswa amefanya uzinduzi huo Machi 16, 2023 kwenye Jukwaa la Pili la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini linaloendelea jijini Arusha linalokutanisha kampuni za uchimbaji wa madini, watoa huduma wa madini kwenye migodi ya madini na Taasisi za Kifedha.

Akizungumzia mfumo huo, Naibu Waziri Kiruswa amesema kuwa mfumo utawezesha kampuni za uchimbaji wa madini na watoa huduma kwenye migodi ya madini kuwasilisha nyaraka mbalimbali kwenye uwasilishaji wa mipango ya ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini na utoaji wa huduma kwa jamii kwenye migodi ya madini kwa njia ya kieletroniki badala ya kutumia nakala ngumu kama ilivyokuwa ikifanyika awali.

Ameongeza kuwa, mfumo pia utarahisisha zoezi la uchakataji wa maombi yanayowasilishwa Tume ya Madini na majibu ya maombi kutolewa kwa wakati na watalaam kutoka Tume ya Madini.

Katika hatua nyingine, akielezea mafanikio ya maboresho ya Sheria ya Madini yaliyopelekea kutungwa kwa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini, Dk. Kiruswa ameeleza kuwa ni pamoja na mabadiliko makubwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kuchochea ongezeko la fursa mbalimbali katika nafasi za ajira na mafunzo, uhaulishaji wa teknolojia, utafiti na maendeleo, matumizi ya huduma na bidhaa zinazotolewa na kuzalishwa na watanzania.

Amefafanua kuwa ajira kwa watanzania katika migodi mikubwa zimeongezeka kutoka 6,668 mwaka 2018 hadi kufikia 15,341 mwaka 2022 pamoja na watanzania wanaopata mafunzo mbalimbali ya kujengewa uwezo wa kufanya kazi ambazo baadhi zilikuwa zinafanywa na wageni ambapo katika kipindi cha mwaka 2022, jumla ya watanzania 8,066 walipatiwa mafunzo mbalimbali katika Sekta ya Madini na kujengewa uwezo katika utendaji kazi ambapo jumla ya Sh bilioni 3.4 zilitumika.

Naibu Waziri Kiruswa ameendelea kueleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na ongezeko la manunuzi ya ndani ya nchi ambapo mwaka 2022 jumla ya Dola za Kimarekani bilioni 2.22 sawa na asilimia 97.4 ya manunuzi yote ya kampuni za madini yalifanyika kwa kutumia kampuni za watanzania, ukilinganisha na Dola za Kimarekani milioni 238.71 sawa na asilimia 46 ya manunuzi yote kwa mwaka 2018 kutumika.

Ameongeza kuwa, kumekuwepo na ongezeko la watoa huduma kwenye migodi ya madini ambapo kwa mwaka 2022 wamefikia 1386 sawa na asilimia 81 ikilinganishwa na mwaka 2018 ambapo kulikuwa na watoa huduma 623.

Naye Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo ameongeza kuwa Serikali kupitia Tume ya Madini bado inaendelea kutoa elimu katika mikoa mbalimbali nchini kuhusu ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini ili wananchi wengi waweze kushiriki kwenye shughuli za utoaji wa huduma kwenye migodi ya madini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles