27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

DK. KIRUMBI: KINGA YA MATENDE, USUBI HAIATHIRI UZAZI

Naibu Mratibu wa Mpango wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele Dk. Edward Kirumbi

 

Na Amina Omari, Tanga

MAGONJWA ya matende, mabusha, minyoo ya tumbo, kichocho, trakoma na usubi ni miongoni mwa magonjwa yasiyopewa kipaumbele na huathiri zaidi jamii na kuidhoofisha.

Inakadiriwa kuwa watu bilioni moja duniani kote duniani wamethirika na magonjwa hayo huku zaidi ya watu bilioni mbili wako hatarini kuugua.

Tafiti mbalimbali zilizowahi kufanyika nchini chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, zinaonyesha kuwa kuna uwezekano wa kuwapo kwa maambukizo ya magonjwa hayo.

Kutokana na tafiti hizo, wizara hiyo imeanza kutekeleza mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele.

Mpango huo wa miaka mitano ulianza kutekelezwa kuanzia mwaka 2012 na unatarajiwa kufikia ukomo wake mwishoni mwa mwaka 2017, ukiwa na lengo la kupunguza au kumaliza maradhi yatokanayo na magonjwa hayo.

Dk. Edward Kirumbi ni Naibu Mratibu wa Mpango wa Taifa wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele nchini, anasema dhumuni la mpango huo ni kuhakikisha magonjwa hayo yanakuwa si tatizo tena.

Anasema magonjwa hayo yameenea zaidi katika ukanda wa kitropiki hususani katika nchi zinazopata joto kwa wingi ambapo Tanzania ni mojawapo.

Anasema mpango huo unalenga kudhibiti magonjwa hayo katika wilaya zote zilizoathirika.

Dk. Kirumbi anabainisha kuwa tafiti za hivi karibuni zilionyesha kuwa zaidi ya watu milioni 47 nchini wako katika hatari ya kupata magonjwa ya matende na mabusha.

“Takribani watu milioni 12.5 walioko katika mikoa 18 na halmashauri 55 wapo hatarini kupata maambukizi ya trakoma na vikope hususani yale maeneo yenye mifugo kwa wingi,” anasema.

Anaongeza kuwa halmashauri 21 zilizoko katika mikoa sita ya Tanga, Singida, Dodoma, Manyara, Rukwa na Geita ipo hatarini kupata maambukizi ya ugonjwa wa usubi.

“Magonjwa haya yamekuwa yakitofautiana kati ya maeneo na maneo, unaweza kukuta mikoa mingine tatizo lipo chini au limekwisha kabisa huku kwingine hali ikiwa mbaya zaidi,’’ anasema Dk. Kirumbi.

Anasema ndio maana mpango huu kwa sasa unatekelezwa nchi nzima ili kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wanapatiwa Kinga.

Anaongeza kuwa lengo ni kuwa na jamii yenye afya bora na Kuondokana na unyanyapaa.

Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa ambao inatekeleza mpango huo kwa kugawa dawa na vifaa tiba katika wilaya zake ili kuhakikisha jamii inapatiwa kinga dhidi ya maradhi hayo.

Mratibu wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele mkoani Tanga, Dk. Rehema Maggid anasema mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2000 katika wilaya tatu kwa ugonjwa wa usubi pekee.

Dk. Maggid anasema waliweza kutoa dawa katika wilaya za Muheza, Lushoto, Korogwe na Mkinga.

Anasema kuwa mwaka 2004 waliweza kuongeza Kutoa dawa tiba kwa magonjwa ya matende na mabusha kwenye wilaya zote za mkoa huo.

Anasema kwa upande wa Wilaya ya Kilindi, wanatoa dawa tiba kwa ugonjwa wa trakoma kwa kuwa ina mifugo mingi ambayo ndio chanzo kikuu cha bakteria wa ugonjwa huo.

Anasema tayari matunda ya utoaji wa dawa hizo yameanza kuonekana ambapo wilaya za Muheza na Lushoto zimeweza kutokomeza magonjwa ya usubi na matende.

Mratibu huyo anasema iwapo wananchi wataweza kumeza dawa, kutakuwa na uwezekano mkubwa wa kudhibiti ugonjwa huo.

Dk. Kirumbi anasema ni vema jamii ikajengewa uelewa kuhusu dhana potofu ya matumizi ya dawa hizo kuwa zina madhara.

“Bado tunafanya uhamasishaji juu ya udhibiti wa magonjwa hayo kwani bado jamii inadhana mbaya ya kuwa unapokunywa dawa kama kinga unaweza Kupoteza uwezo wa kuzaa, jambo ambalo si kweli,” anasema.

“Jamii bado inaamini kuwa dawa hizo zina madhara lakini bado tunajitahidi kuongeza uhamasishaji hadi ngazi za kaya ili kuweza kupata ufumbuzi kwa haraka,” anaongeza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles