NA VERONICA ROMWALD- DAR ES SALAAM
MADAKTARI Bingwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu, Ubongo na Uti wa Mgongo Muhimbili (Moi), bado wanaendelea kufuatilia kwa ukaribu hali ya afya ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla.
Dk. Kigwangalla amelazwa hospitalini hapo kwa matibabu ya kibingwa baada ya ajali aliyopata Agosti 3, mwaka huu huko mkoani Manyara, huku Ofisa Habari wa Wizara hiyo, Hamza Temba alifariki dunia papo hapo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Uhusiano wa Moi, Patrick Mvungi, alisema afya ya Dk. Kigwangalla inaendelea kuimarika.
“Bado tunaye, amelazwa wodini, hali yake inaendelea kuimarika. Lakini madaktari hawajampatia ruhusa, wanaendelea kufuatilia zaidi hadi watakapojiridhisha ndipo watamruhusu kwenda nyumbani na ataanza kuhudhuria kliniki kama mgonjwa wa nje,” alisema.
Agosti 12, mwaka huu, Dk. Kigwangalla alifanyiwa upasuaji wa mkono wake ambao ulivunjika kutokana na ajali aliyoipata.