29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

DK. KAWARI AKARIBIA KURITHI MIKOBA YA BOKOVA UNESCO

PARIS, UFARANSA


ALIYEKUWA Waziri wa Utamaduni wa Qatari, Dk. Hamad Bin Abdul Aziz Al Kawari (68) anapewa nafasi kubwa ya kumrithi ukurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Irina Bokova.

Mchakato huo wa awali unaotokana na muda wa Bokova kuliongoza shirika hilo kumalizika ulifanyika Aprili 24 mwaka huu kwa usaili uliohusisha wagombea kutoka nchi za Qatar, Misri, Vietnam, Ufaransa, China na Lebanon.

Katika mchuano huo wa kwanza, Dk Al Kawari aliibuka mshindi akifuatiwa na wagombea kutoka China na Ufaransa.

Hata hivyo, Dk. Al Kawari anapewa nafasi kubwa ya kushinda kinyang’anyiro hicho kwa vile Ufaransa na China zilishatoa watu walioliongoza shirika hilo hivi karibuni.

Taarifa zilizopatikana juzi kutoka makao makuu ya UNESCO mjini hapa, zinasema kwa mujibu wa taratibu, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO akishachaguliwa, hufuatiwa na uchaguzi mwingine wa manaibu wakurugenzi wakuu watatu wanaotakiwa kuthibitishwa na Baraza la Utendaji la shirika hilo.

Manaibu wakurugenzi hao, hushughulika na Bara Ulaya,  Amerika na Bara la Afrika, Mashariki ya Kati na Asia.

Ushindi wa Dk. Al-Kawari unaweza kuinufaisha Tanzania kutokana uhusiano mzuri baina yake na Qatari, ambayo ina ubalozi wake mjini Dar es Salaam.

Endapo Dk. Al-Kawari, ambaye ni mbobezi katika diplomasia ya dunia atashinda kiti hicho, atakuwa raia wa kwanza kutoka nchi za Kiarabu  kuongoza shirika hilo.

Alianza kazi mwaka 1972, kama ofisa wa ubalozi nchini Lebanon, ambapo baadaye mwaka 1974 akateuliwa kuwa balozi wa Qatari nchini Syria, nafasi aliyodumu nayo kwa miaka mitano.

Mwaka 1979 aliteuliwa kuwa balozi nchini Ufaransa, huku akiiwakilisha pia katika nchi za Italia, Uswisi, Ugiriki na baadaye kuwa mmoja wa wajumbe wa Qatari, UNESCO kuanzia mwaka 1979 hadi 1984.

Mwaka 1984 hadi 1990, alikuwa balozi wa Qatari nchini Marekani, Mexico na Venezuela.

Mwaka 1992 alirudi Qatari na kuteuliwa kuwa Waziri wa Habari na Utamaduni, nafasi aliyodumu nayo hadi mwaka 2007 kabla ya kubadilishiwa wizara na kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Urithi.

Dk. Al Kawari, ambaye anazungumza lugha tatu za Kiarabu, Kifaransa na Kiingereza kwa ufasaha kwa sasa ni mshauri wa masuala ya utamaduni kwa kiongozi wa Qatari, Sheikh Tamim Bin Hamad Al Thani.

Ameandika vitabu kadhaa zikiwamo“Dialectics of Conflicts and Settlements” (2001) na “The Deficient Knowledge” (2005) na amekuwa akiandika makala mbalimbali katika majarida ya kimataifa.

 Al-Kawari ana shahada ya uzamivu katika Sayansi ya Siasa aliyoipata mwaka 1990 kutoka Chuo Kikuu cha Stony Brook, New York nchini Marekani.

Shahada yake ya uzamili aliipata mwaka 1980 kutoka Chuo Kikuu cha Sorbonne, Ufaransa.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles