Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Imeelezwa kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan inautambua mchango wa mwalimu katika kujenga maendeleo ya Taifa.
Hayo yamebainishwa Jumapili Oktoba 9, 2022 na Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko wakati wa Sherehe ya Siku ya Mwalimu Duniani iliyoadhimishwa katika wilaya ya Bukombe na kuhudhuriwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda mkoani Geita.
Ameongeza kuwa, mchango wa walimu nchini ni mkubwa katika utoaji wa elimu. Amesema mwalimu ni msingi katika kujenga uchumi.
Naye, Prof. Mkenda amesema katika kusheherekea Siku ya Mwalimu Duniani Serikali itaandaa sherehe hizo ili zifanyike katika wilaya Bukombe Mwaka 2023.
Aidha, ameahidi kujenga Chuo cha Ufundi Stadi cha VETA katika wilaya ya Bukombe ili kurahisisha kutoa msaada kwa wanachi wa Bukombe na Mkoa wa Geita.
Hafla hiyo imeandaliwa na Chama cha Walimu wilaya ya Bukombe imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ili kusheherekea kwa pamoja siku hiyo muhimu ya mwalimu duniani.