Na Esther Mnyika , Mtanzania Digital
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ameonya dhidi ya unyanyasaji wa watu wenye ulemavu, akisisitiza kuwa Serikali itachukua hatua kali kwa wahusika wa vitendo hivyo. Alitoa kauli hiyo, Desemba 3, 2024, jijini Dar es Salaam, alipomwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu duniani.
“Hatuwezi kuvumilia kuona vitendo vya unyanyasaji, mauaji, au biashara ya viungo vya watu wenye ualbino. Serikali itakula sahani moja na wahusika,” alisema Dk. Biteko.
Katika tukio hilo, Mpango Kazi wa Taifa wa Haki na Ustawi wa Watu Wenye Ualbino na Mkakati wa Taifa wa Teknolojia Saidizi ulizinduliwa. Dk. Biteko alisisitiza utekelezaji wa mipango hiyo, akielekeza halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu.
Waziri wa Nchi, Ridhiwan Kikwete, alibainisha kuwa mkakati huo unalenga kuondoa unyanyapaa na kuboresha fursa kwa watu wenye ulemavu. Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alieleza kuwa zaidi ya watu 600,000 wenye ulemavu wanajipatia kipato kupitia biashara ya bajaji.
Maadhimisho hayo yaliambatana na shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuwawezesha watu wenye ulemavu na kujenga jamii jumuishi.