27.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 27, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Biteko awataka wafanyabiashara kuwafichua wanaowakwamisha

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko amezitaka taasisi mbalimbali kuacha vikwazo kwa wafanyabiashara badala yake ziwe wezeshi ili kukuza sekta hiyo muhimu nchini.

Amesema andiko la Blueprint limeainisha changamoto mbalimbali zinazokwaza maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara nchini na Serikali inaendelea kuhakikisha changamoto zinazokabili biashara na uwekezaji ikiwemo sekta ya viwanda zinatatuliwa.

Akizungumza Septemba 26,2024 kwa niaba ya Makamu wa Rais wakati akifungua Maonesho ya Kimataifa ya Viwanda Tanzania (TIMEXPO), amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya biashara ili kukuza uchumi wa nchi na viwanda.

“Kulikuwa na taasisi sita sitazitaja, zilikuwa kikwazo kwa wafanyabiashara lakini sasa zimebadilika zimekuwa wezeshi, tuambiane ukweli kwamba fulani ndiyo anatukwamisha tumjue, tukimjua tutafute namna ya kumsaidia.

“Serikali inaendelea kuhakikisha changamoto zinazoikabili biashara na uwekezaji ikiwemo katika sekta ya viwanda zinaendelea kutatuliwa,” amesema Dk. Biteko.

Aidha amewataka wadau wa viwanda kuendelea kutoa maoni katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 kwa kuwa sekta hiyo ni kiungo muhimu cha ajira.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Paul Makanza, amesema licha ya sekta ya viwanda kukua kutoka asilimia 8.1 (2000 – 2004) hadi asilimia 11.1 (2020 – 2024) lakini mchango wake katika Pato la Taifa umepungua kutoka asilimia 10.1 hadi kufikia asilimia 7.8.

“Mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa bado ni mdogo, malengo tunataka tufikie angalau asilimi 12, mauzo ya nje bado ni finyu lakini bado kuna fursa ya kutengeneza bidhaa za Tanzania kwa ajili ya kuuza nje,” amesema Makanza.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albart Chalamila, amesema bado kuna changamoto ya uingizwaji wa bidhaa katika njia zisizo rasmi ambazo zimekuwa tishio kwa viwanda vya ndani huku akiyataja maeneo zinakopita kuwa ni Mbweni, Kunduchi, Bagamoyo na Pembamnazi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amesema maonesho hayo ni fursa kwa wazalishaji na taasisi wezeshi kutangaza bidhaa na kujifunza teknolojia mpya ili waweze kutengeneza bidhaa zenye ushindani.

“Tunahitaji nguvu ya pamoja kati ya Serikali na wadau binafsi ndiyo maana CTI imetambua hilo na kuunga mkono juhudi za Serikali…tunataka kuona hamasa zaidi kwa wazalishaji wadogo,” amesema Kigahe.

Maonesho hayo yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa CTI na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) yalianza mwaka 2023 kwa kushirikisha washiriki 79 lakini mwaka huu wameongezeka na kufikia 250 zikiwemo kampuni kutoka nje.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles