27.7 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Biteko atoa onyo wanaoshusha ubora dhahabu Geita

*Aagiza kufuta leseni kwa wote wanaoshusha dhahabu ubora

*Asema Watumishi, Wafanyabiashara wanaohusika na mchezo huo hawapo salama

*Serikali kuweka mfumo katika masoko kubaini watakaopunguza ubora wa madini

Na Mwandishi Wetu, Geita

Siku chache baada ya Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko kuagiza wafanyabiashara wa Madini kuacha kushusha ubora wa dhahabu (purity) katika Masoko ya Madini ametoa onyo kwa wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja.

Dk. Biteko, ametoa onyo hilo juzi katika Soko kuu la Dhahabu Mkoani Geita baada ya kufanya ziara ya kushtukiza wafanyabiashara na watumishi ili kubaini wanaoshusha ubora wa dhahabu katika soko hilo.

Amesema, Serikali itafuta leseni za wafanyabiashara wasio waaminifu wa madini ya dhahabu na hatua za kisheria zitafuatwa kwa wote wanaoshusha dhahabu katika masoko ya madini.

“Kitu cha kwanza tulichokubaliana tukibaini mmoja anafanya michezo hiyo tutakunyang’anya leseni ili ukafanye biashara nyingine ambayo unaweza kufanya ujanja ujanja, lakini biashara ya madini kila mtu tunataka afanye kwa haki, kulipa kodi yako sahihi, wateja wako uwalipe sahihi,” amesema Dk. Biteko.

Pia, ametoa onyo kwa maafisa wa Serikali wanaoshiriki katika mchezo huo wa kushusha ubora dhahabu. Amesema tayari wamekamilisha kupata orodha yao kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi.

Vile vile, Serikali mkakati nchi nzima kwa ajili ya kufuatilia wale wachache ambao wanadanganya kwenye ubora wa dhahabu ili kukomesha mchezo huo.

Ameongeza hakuna haja ya kushusha ubora dhahabu kwa kuwa Serikali imetengeneza mazingira mazuri ya wafanyabiashara wa madini nchini kufanya biashara kwa uwazi na weledi mkubwa.

“Kuna kitu gani Serikali haijaleta, kuna jambo lipi mlilo omba Serikali haijafanyia kazi, mmesema TASAC tumeshughulika nayo, mlisema masoko tumeshughulika nayo, mlisema mirabaha tunashughilika nayo na kila mnachoomba Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anawapeni,” amesisitiza Dk. Biteko.

Dk. Biteko amesema pia, Serikali imeweka mazingira mazuri ya wafanyabiashara wa madini ili Serikali iweze kupata mapato makubwa yatokanayo na shughuli za madini badala ya kutorosha madini au kushusha ubora.

Aidha, amewapongeza wafanyabiashara wa dhahabu wanaoendelea kufanya biashara. Amesema Serikali itaendelea kuwalinda ili wafanye biashara kwa amani, walipe kodi, Serikali ipate mapato ili Sekta ya Madini ikue kwa pamoja.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula amewataka wafanyabiashara hao kuzingatia maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Madini kwa niaba ya Serikali.

Prof. Kikula ameongeza, wafanyabiashara kuwa wakweli katika biashara zao ili Sekta ya Madini iweze kukua. Amewataka kuacha mchezo huo mara moja kwani watatambulika wote watakaojihusisha na ushushaji dhahabu ubora katika masoko yote ya madini.

Ziara ya Kushtukiza ya Dkt. Biteko katika Soko la Madini Geita imelenga kutoa onyo kwa wale wanojihusisha na kushusha ubora wa dhahabu kwa kupunguza asilimia chache za dhahabu kitendo kinachofanywa na baadhi ya watumishi wachache pamoja na wafanyabiashara wa madini ili kumuibia mteja au Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles