28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Biteko ashuhudia utiaji saini mikataba miwili ya gesi

*Ni wa mauziano ya gesi asilia na ujenzi wa miundombinu midogo

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko leo ameshuhudia uwekaji saini mkataba wa mauziano ya gesi asilia itakayozalishwa katika eneo la Ntorya Kitalu cha Ruvuma.

Pia uwekaji saini hati ya makubaliano ya kuanzisha mahusiano ya kujenga miundombinu ya kusambaza gesi asilia kwa teknolojia ya miundombinu midogo ya kuibadilisha kuwa kimiminika (Mini-LNG).

Hafla ya utiaji saini imefanyika Januari, 10 2024, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo mkataba wa mauziano ya gesi asilia itakayozalishwa eneo la Ntorya umesainiwa kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kampuni ya ARA Petroleum ya Oman na Ndovu Resources ya Uingereza.

Dk. Doto Biteko Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Hati ya Makubaliano kwa ajili ya kuanzisha mahusiano ya kujenga miundombinu ya gesi asilia imesainiwa kati ya TPDC na Kampuni ya KS Energy.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Biteko amesema kuwa, mkakati wa Wizara ya Nishati ni kuhakikisha kuwa inasimamia ipasavyo Sera ya nishati ya mwaka 2015.

Amesema kuwa, lengo la nchi ni kuwa na nishati inayotokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo jua, upepo, gesi na maji ili gesi asilia iliyopo itumike pia kwa kiasi kikubwa kwenye maeneo mengine kama viwanda na majumbani badala ya kutumika kwa kiasi kikubwa kwenye umeme na pia kupunguza matumizi ya mafuta.

“Mkakati wetu ni kubadilisha suala hili la gesi asilia kutumika zaidi kwenye umeme ambayo ni takriban asilimia 80, tunataka kuwe na nishati mchanganyiko nchini ili gesi itumike kwenye viwanda na majumbani na pia tupunguze utegemezi wa mafuta,” amesema Dk. Biteko.

Ameongeza kuwa, TPDC sasa wana mkakati utakaowezesha kuwa na mgawanyo wa matumizi ya nishati hiyo ambapo matumizi kwenye umeme itakuwa asilimia 38, majumbani na viwandani itakuwa asilimia 32 na asilimia 10 itabaki majumbani tofauti na ilivyo sasa ambapo matumizi ya gesi viwandani na majumbani ni asilimia 28 na asilimia iliyobaki kwa kiasi kikubwa inaenda kwenye umeme.

Kuhusu hati iliyosaniwa ya miundombinu midogo ya LNG, Dk. Biteko amesema kuwa nchi ina kilometa za mraba 945,000 na kwamba pamoja na uwepo wa Bomba la Gesi Asilia nchini njia rahisi ya kufanya gesi iwafikie watu wengi ni kuigeuza kuwa kimiminika na kusafirisha kwa magari kwenda kwenye maeneo ambayo watu watatumia.

Amesema kuwa, Serikali ipo tayari kushirikiana na wawekezaji hao ili kuwafikishia wananchi nishati ya uhakika kutoka vyanzo mbalimbali huku akitolea mfano utekelezaji wa mradi wa megawati 50 unaotokana na jua wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga na ujenzi wa miradi mingine ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme.

Ameeleza kuwa, Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan anafuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya nishati nchini kwani anachotaka ni watu wapate umeme wa uhakika pamoja na nishati nyinginezo.

Vilevile, amesema kuwa, Serikali haitaki urasimu katika utekelezaji wa mipango inayojiwekea kwani nia ni kwenda na wakati na kufanya vitu vitokee kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha badaye.

Amesema kuwa, Serikali inaangalia vitu muhimu ambavyo vitaondoa watu kwenye umaskini kwa haraka zaidi ikiwemo uwepo wa miundombinu ya barabara, anga, reli, bandari na uwepo wa nishati ya uhakika ambapo kwa upande wa Wizara ya Nishati, zinafanyika kila jitihada ili kuwe na nishati ya kutosha na ya uhakika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema kuw miradi hiyo ina umuhimu mkubwa ikiwemo katika mikoa ambapo rasilimali hiyo inazalishwa na kwamba watahakikisha wanaisimamia kwa maendeleo ya Mtwara na nchi kwa ujumla.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame amesema kuwa, mkataba wa mauziano ya gesi asilia uliosainiwa leo utawezesha kuongeza gesi iliyogunduliwa nchini ambapo mradi huo unategemea kuzalisha kiasi cha kuanzia futi za ujazo milioni 60 kwa siku hadi kufikia futi za ujazo milioni 140 kwa siku katika kipindi cha miaka mitatu.

Ameongeza kuwa, kukamilika kwa mkataba huu kutawezesha shughuli nyingine za uendelezaji kufanyika kama vile, ujenzi wa miundombinu ya kukusanya gesi kutoka visimani, ujenzi wa miundombinu ya kukusanya gesi kutoka visimani, ujenzi wa miundombinu ya usafishaji wa awali ikiwemo kutoa maji na ujenzi wa bomba la kilometa 34 la kusafirisha gesi asilia hadi kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo Msimbati, Madimba mkoani Mtwara.

Ameeleza kuwa, katika kitalu cha Ruvuma gesi iliyogunduliwa na kuhakikiwa ni futi za ujazo bilioni 1.6.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles