26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

DK. BILAL ASHTUSHWA MAMBUKIZI YA UKIMWI

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM


MAKAMU wa Rais mstaafu, Dk. Mohamed Gharib Bilal, ameonesha kushtushwa kwake na  kasi kubwa ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi katika mikoa mine.

Akizungumza mwishoni mwa wiki mjini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Kili Challenge kwa mwaka 2017 ambayo inaandaliwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), yenye lengo la kuchangia fedha  za mapambano ya ugonjwa huo, Dk. Bilal aliwataka wadau, Serikali na mashirika mengine kuongeza nguvu kutoka na mikoa hiyo kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi.

Aliitaja mikoa hiyo na asilimia zake kwenye mabano, kuwa ni Njombe (14.8), Mbeya (9), Iringa (9.1), Manyara (1.5) lakini takwimu za ndani ya mkoa huo, zinaonesha eneo la Mirerani ambako maambukizi pekee yamefikia asimilia 16.

“Nimeshtushwa na kiwango kikubwa  cha maambukizi ya virusi vya Ukimwi katika mikoa hii, wekeni nguvu ya ziada haraka, Taifa linapoteza nguvu kazi na kubaki na watoto yatima wengi.

“Ninyi Tacaids (Tume ya Kudhibiti Ukimwi), hali ni mbaya naamini kwa mikakati yenu mlionayo, ni vizuri zaidi mkaelekeza nguvu ya ziada maeneo haya, maana mkichelewa tutazidi kuumia kama Taifa,”alisema Dk. Bilal.

Alisema katika  ugonjwa huo, makundi makubwa ambayo yameathirika zaidi na asilimia zao kwenye mabano ni makahaba (26), wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja (22),watumiaji wa dawa za kulevya wanaojidunga sindano (15), madereva wa malori makubwa, wafungwa, wavuvi na wasakara ajira (5), huku vijana wa miaka 16 hadi 24 maambukizi yameongeza mara dufu.

“Takwimu zinaonyesha asilimia 70 ya maambukizi haya yanatoka kwa wasichana, natoa raia kwa wadau kuweka nguvu vijana wetu ili waweze kujitambua juu ya tatizo hili. Tukifanya hivi tutakuwa tumewaunga mkono wenzetu wa GGM ambao kwa miaka 16 sasa, wanaendesha kampeni ya kupanda Mlima Kilimanjaro,”alisema.

Alisema kumekuwa na mafanikio ya kupambana na Ukimwi kati ya mwaka 2010 hadi 2015, kiwango kipya cha maambukizi ya VVVu kilishuka kwa asilimia 20, japo watu 48000 wameambukizwa mwaka 2015.

Alisema zaidi ya nusu ya watu wanaoishi na VVU wanapata dawa, hadi mwisho mwaka 2015, watu milioni 1.4, kati yao 80,000 walikuwa wanapata dawa za kufubaza ugonjwa huo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa GGM, Richard Jordinson alisema wataendelea na mkakati huo ambao umeonekana kuwa na manufaa makubwa kwa Taifa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids),Dk. Leonard Maboko alisema juhudi zinazofanywa na GGM, zitasaidia VVU na Ukimwi kupungu na kufikia lengo la asilimia 0.3 mwaka 2030.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles