23 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Bashiru azungumzia mwelekeo wa wapiga kura

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, amesema kutokana na mwenendo wa siasa ulivyo nchini, huenda wanasiasa wakasababisha idadi ya wapigakura ikashuka katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaokuja.

Akizungumza na wanahabari katika kipindi cha ‘Tujadiliane’ kinachoendeshwa na UTPC jana jjini Dodoma, Dk. Bashiru alisema iwapo siasa hazitapewa taswira nzuri, upo uwezekano wa idadi ya wapigakura kushuka tofauti na ilivyozoeleka.

Alisema Tanzania imekuwa katika rekodi nzuri ya watu wanaojitokeza kupiga kura ambao wamekuwa wakifikia zaidi ya asilimia 70 ya waliojiandikisha, lakini uchaguzi wa hivi karibuni unaonesha kuna mabadiliko kwa idadi hiyo.

“Ukiangalia rekodi, kadiri tunavyochafua siasa zikawa za uongo uongo na mbwembwe, matokeo yake idadi ya wapigakura inashuka. Hatujawahi kukosa chini ya asilimia 70 ya waliojiandikisha ambao wanajitokeza kupiga kura, tuna rekodi nzuri ya kitaifa, lakini ukiangalia mwelekeo idadi inashuka, hali ambayo siyo nzuri,” alisema.

Dk. Bashiru alikuwa akizungumzia namna CCM inavyojipanga kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu na namna anavyoona mwelekeo wa kisiasa katika utaratibu wa usimamizi wa kura za maoni na upigaji kura.

Alisema ni vyema wanasiasa wajenge utamaduni wa kuhamasisha umma na kuonyesha kuwa kura ni sehemu ya kuleta mabadiliko, hivyo kujua umuhimu wao kushiriki katika upiaji kura.

Suala jingine alisema ni kwa wanasiasa kuacha ulaghai wakati wa kampeni na waahidi mambo ambayo wana uhakika watayatekeleza kwa kuwa ahadi hewa pia ni chanzo cha kuwakatisha tamaa wapigakura.

Dk. Bashiru alisema ni vyema pia wanasiasa watambue kuwa hali ya siasa ya sasa si rahisi kama ilivyokuwa miaka iliyopita kwa kuwa idadi ya vijana ni kubwa na uelewa wa watu umeongezeka, hivyo suala ambalo hataki kuona likitokea ni la wananchi kukata tamaa ya uchaguzi kwa sababu ya matendo ya wanasiasa.

Alisema uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa una thamani kubwa kuliko nyingine kwa sababu viongozi watakaochaguliwa ndio walio karibu kabisa na wananchi na ndio wanaotatua matatizo yao ya kila siku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles