Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk.Bashiru Ally amefanya mazungumzo na Balozi wa China nchini,Wang Ke kujadiliana namna ya kusaidiana katika sekta za uwekezaji, biashara, afya, elimu pamoja na eneo la Vyuo vya Ufundi.
Akizungumza leo, Desemba 12 , Makao Makuu ya CCM Dodoma (White House), Dk.Bashiru amesema mazungumzo hayo yalijikita namna ya kuboresha na kusaidiana na Serikali ya China kuboresha sekta za afya, elimu, biashara, uwekezaji na katika vyuo vya ufundi.
“Mazungumzo yalikuwa marefu kidogo na agenda zilikuwa ni namna ya kusaidiana na kuboresha sekta za uwekezaji, biashara na sekta za afya na elimu na vyuo vya ufundi hasa katika eneo la ujuzi,”amesema Dk. Bashiru.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini,Wang Ke amesema CCM kina historia kubwa na China hivyo amefika Makao Makuu ya CCM kwa lengo la kukipongeza Chama hicho kwa kupata ushindi mkubwa pamoja na Mwenyekiti wa Chama hicho, Dk. John Magufuli kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.