28.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 22, 2023

Contact us: [email protected]

Dk. Bashiru amshukia Makonda, aomba msamaha

Upendo Mosha -Moshi

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amejikuta katika wakati mgumu baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, kumwombea msamaha hadharani kutokana na kauli yake iliyotafsiriwa kuwa ni ya kuwakashifu Wachaga.

Sakata hilo lilianzishwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alipokuwa akitoa salamu za rambirambi katika ibada ya kumuaga aliyekuwa Mwenyekiti wa Makapuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi, iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Usharika wa Moshi Mjini.

Akitoa salamu hizo, Mbowe alisema; “kumekuwa na kauli ambazo sitaweza kuzivumilia ambazo zinaonyesha ubaguzi, kwamba eti kabila gani halina uwezo wa kuwapenda walemavu, jambo hili si la kufumbia macho na tusikubali kugawanywa.

“Tunastahiki kupendana na kupinga vitendo na kauli za kibaguzi, hasa pale anaposimama kiongozi na kuzitoa, mimi suala la kiongozi kusema kabila flani halitoi misaada kwa walemavu sijalipenda na ni kauli za kinafiki, tuungane kupinga hili.”

Kauli hiyo pia iliungwa mkono na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick Shoo ambaye kwenye mahubiri yake alikemea viongozi vijana akisema waache kujitutumua kama chatu.

Pia alisema kauli za kibaguzi na za kugawa watu ni vyema zikakemewa kwani ni dhambi mbaya ambayo inabidi watu watubu kwa ajili yake.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Bashiru akitoa salamu za rambirambi za CCM, alisema ataendelea kuwa mwanafunzi wa mafundisho ya Dk. Shoo.

Dk. Bashiru alikubaliana na jinsi Dk. Shoo alivyokemea viongozi na hasa wale vijana, huku akisema kwa sasa wanavuna matunda ya kutoandaa viongozi na kwamba anamwombea msamaha Makonda kwa kauli zake.

“Tunahitaji kuwasaidia vijana wetu katika uongozi. Ni mara ya pili sasa namkemea Makonda hadharani kwa kauli zake, ila sasa ameanza kubadilika,” alisema Dk. Bashiru.

Mara baada ya kauli hiyo, Dk. Shoo alimwita Makonda madhabahuni ili amshike mkono.

Hata hivyo kwa kadiri dakika moja Makonda alionekana kusita kunyanyuka katika kiti chake huku akitikisa kichwa.

Wakati huo waliokuwa wameketi karibu naye walionekana kumshauri na hatimaye alinyanyuka na kwenda mbele ya kanisa.

Akiwa hapo, baada ya askofu kumshika mkono, alionekana kusita kutoka huku akitaka kuzungumza jambo na kutaka Mbowe pia aitwe.

Mbowe alipoitwa walizungumza kidogo na kushikana mikono kisha Makonda akaruhusiwa kuzungumza.

Makonda alisema watu waliitafsiri vibaya kauli yake, na kwamba hakuwa na lengo la ubaguzi kama ilivyochukuliwa.

“Nafurahi kwamba tumekutanishwa mbele ya askofu hapa na kaka yangu Mbowe kwa jambo ambalo limezua minong’ono, lakini sikuwa na maana ambayo imetafsiriwa, nilikuwa nasifu Mchaga katikati ya Wachaga,  sikueleweka, naomba mnisamehe sana,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,079FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles