24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 29, 2023

Contact us: [email protected]

Dk. Bashiru Ally amtaka Waziri Mkuu kusimamia watendaji

ELIZABETH HOMBO -DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, amewaonya wakuu wa mikoa ya Morogoro, Dk. Stephen Kebwe na John Mongella wa Mwanza, akiwataka kusimamia shughuli za Serikali katika mikoa yao, huku akimtaka Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kusimamia watendaji.

Alitoa kauli hiyo jana wakati wa kilele cha maonyesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa viwanja vya Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.

Pamoja na mambo mengine, Dk. Bashiru alisema Dk. Kebwe alishindwa kumshughulikia mkurugenzi wa halmashauri ambaye hakumtaja kwa jina, akidai alitumia Sh milioni 60 zilizotolewa kwa matumizi maalumu kununulia dawa ya mchwa.

Mbali na hilo, Dk. Bashiru alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka akisema ni miongoni mwa wakuu wa mikoa wachapakazi nchini.

“Ninachosisitiza hapa ni kufanya kazi kama timu, sasa pale Morogoro kuna mkurugenzi mmoja amepewa fedha Sh milioni 60, RC hakushughulika na mkurugenzi huyu hadi Rais (John Magufuli) alipoingilia kati. Sasa RC wa Morogoro pokea ujumbe wangu,” alisema.

Pia alimtaka Mongella kumsimamia na kumbana mkurugenzi wa halmashauri ya Sengerema ambaye alishindwa kutoa kiwango cha bajeti ya miundombinu ya barabara.

“Tatizo kama hilo lipo pia Sengerema, mkurugenzi anaulizwa kiwango cha bajeti ya miundombinu ya barabara anakuwa bubu.

“Najua haya kwa Simiyu chini ya uongozi wa Mtaka yasingetokea kwa sababu ana ushirikiano mzuri na wenzake.

“Ninawasihi msisubiri Rais ndio aje kufanya maamuzi kwenye maeneo yenu,” alisema Dk. Bashiru.

Kutokana na hayo, Dk. Bashiru aliwataka wakuu wa mikoa yote nchini pamoja na watendaji wengine wa Serikalim kufanya kazi kwa ushirikiano pamoja na uwajibikaji.

Alitangaza kuondoa kauli yake kuhusu migogoro miongoni mwa viongozi wa CCM na Serikali mkoani Mara, aliyosema ilikuwa inakwamisha maendeleo, aliyoitoa wakati wa kilele cha Nanenane mwaka jana.

“Nawapongeza viongozi wa Mara kuwa hali sasa iko shwari. Naondoa kauli yangu ya mwaka jana kuhusu mkoa wa Mara,” alisema Dk. Bashiru.

MIKOA INAYOONGOZA KWA MIGOGORO

Alitaja mikoa ya Mara, Arusha na Dar es Salaam kuwa ni miongoni mwa inayoongoza kwa migogoro miongoni mwa viongozi, akisema inakwamisha utekelezaji wa ilani ya CCM huku akiwaagiza viongozi wa mikoa hiyo kujirekebisha.

WAZIRI MKUU

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizitaka Wizara ya Kilimo, Viwanda na Biashara, Uvuvi na Mifugo kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, kutengeneza mkakati wa kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini. 

Majaliwa ambaye alimwakilisha Rais Magufuli katika maonyesho hayo, alivitaja viwanda hivyo kuwa ni pamoja na vya nyuzi, nguo, ngozi, maziwa, minofu, nyama, kubangua korosho, kutengeneza unga, mafuta ya kula, sabuni, usindikaji wa matunda na mbogamboga.

VYAMA VYA USHIRIKA  

Vilevile aliagiza kuimarishwa kwa vyama vya ushirika ili kumwezesha mkulima kuendelea kumiliki zao lake hatua hatua ya kuuza sokoni.

“Katika kuimarisha vyama vya ushirika, rai yangu kwa mashirika yote nchini hakikisheni mnaendeleza ushirika kwa sababu ndiyo njia pekee ya ukombozi ambayo inawakutanisha wakulima pamoja, ni rahisi kufikisha malipo ya biashara,” alisema. 

Alisema mfano ulioonyeshwa katika zao la kahawa kupitia Chama Kikuu cha Ushirika Kagera (KCU), ni mzuri ambapo wanamiliki asilimia 100 ya kiwanda cha kukoboa kahawa (Bucop), pamoja na asilimia 54 ya kiwanda cha kuzalisha kahawa – Tanganyika Instant Coffee (Tanica).  

“Kwa upande wa pamba, Nyanza Cooperative Union (NCU) walianza vizuri kwa kumiliki viwanda vinane vya kuchambulia pamba. Tunataka jitihada za namna hii zianzishwe katika shughuli za wakulima wetu na zilizopo ziimarishwe,” alisema Majaliwa.  

Katika hilo, aliitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na wadau, kufanya tathmini kwenye vyama vya ushirika vinavyomiliki viwanda ili kubaini hali ilivyo kwa sasa na kuweka mikakati ya kuvifufua na kuviongezea uwezo.

 “Kumbukeni kuwa kila mmoja wetu akitimiza wajibu wake ipasavyo, maendeleo ya viwanda yanawezekana, ajira zitapatikana, uhakika wa chakula na lishe bora itakuwepo na sote kwa pamoja tutasonga mbele kufikia nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” alisema.

MFUMO WA MAZAO 

Katika hatua nyingine, Majaliwa alizindua mfumo wa uuzaji wa mazao kupitia Soko la Bidhaa (TMX), ambao kuanzia mwakani utaanza kutumika kununua na kuuza baadhi ya mazao ndani na nje ya nchi.

Alisema mfumo huo utawahakikishia wakulima upatikanaji wa malipo kwa muda mfupi na wanunuzi kuwa na uhakika wa kupata mazao, bidhaa zenye ubora na zinazotosheleza mahitaji yao.  

“Baadhi ya mazao tunayotarajia kuanza nayo ni pamoja na dengu, choroko, mbaazi, ufuta, korosho, kahawa na kokoa.

“Mfumo huu utasaidia upatikanaji wa masoko ya uhakika na kwa uwazi na hivyo kuifanya nchi ijulikane kimataifa juu ya uzalishaji wa mazao hayo na mengine,” alisema.  

Alisema katika kuhakikisha mafanikio yanapatikana kwenye sekta za kilimo, viwanda na biashara, ni lazima soko la bidhaa lipewe ushirikiano ngazi zote.

“Taratibu zote za uendeshaji wa biashara hiyo zikamilike kwa ushirikiano wa vyama vya ushirika, Tamisemi, Wakala wa Stakabadhi Ghalani na Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Fedha na Mipango.

“Pia elimu kwa wadau wote itolewe kwa muda wote ili kuwaandaa washiriki wa mnyororo mzima wa thamani za mazao.

“Napenda kusisitiza kuwa kuanza kufanya kazi kwa mfumo huu ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ibara namba 22(g)(ii) ya 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17– 2020/21) na Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II),” alisema.

Vilevile, Majaliwa alizindua mfumo mwingine wa kielektroniki wa kusimamia biashara za kilimo (Agricultural Trade Management Information System – ATMIS).

“Mifumo hii inalenga kuongeza ufanisi wa shughuli mbalimbali za kuendeleza sekta za kilimo nchini na kuimarisha biashara ya mazao na bidhaa za kilimo,” alisema.

Akizungumzia changamoto, alisema ni pamoja na kuwepo kwa mlolongo mrefu wa kupata vibali na leseni za uwekezaji na biashara, na wateja kulazimika kufuata vibali hivyo ofisi za taasisi zilizopewa mamlaka ya kutoa leseni na vibali hivyo.  

“Niwapongeze Wizara ya Kilimo na Taasisi ya TradeMark East Africa kwa kusanifu na kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa kutoa vibali, leseni na huduma za malipo kwa wafanyabiashara,” alisema.

Aliitaka Wizara ya Kilimo kusimamia utekelezaji wa mfumo huo ili lengo linalotarajiwa na Serikali, hususani kurahisisha biashara liweze kufikiwa.

“Pia taasisi na idara zote zinazotumia mfumo huo zihakikishe zinatoa elimu kwa watumiaji na wadau wote wa mfumo kwa lengo la kuondoa urasimu katika kuwahudumia wateja,” alisema. 

Alisema katika kutekeleza mkakati wa kuimarisha mfumo wa biashara za mazao nchini, Serikali imetengeneza mfumo wa kielektroniki wa utoaji wa leseni, vibali na malipo ya huduma (ATMIS) ili kurahisisha biashara za mazao ya kilimo. 

Aliwaagiza viongozi wa Wizara ya Kilimo, kuhakikisha wanashirikiana na viongozi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, kusimamia mifumo hiyo sanjari na kupambana na wanunuzi nje ya mifumo iliyokusudiwa.

NYAKABINDI KUWA KITUO CHA MAONYESHO

Majaliwa pia aliagiza wizara zote na taasisi zinazohusika na maonyesho ya kilimo, kujenga majengo ya kudumu katika viwanja vya maonyesho ya wakulima Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.

“Tunataka viwanja hivi vya Nyakabindi kuwa kituo cha kudumu cha mafunzo ya kilimo, lazima tuonyeshe kwa vitendo. Wataalam lazima wawepo hapo kusimamia mashamba darasa na kutoa mafunzo kwa wakulima wanaotembelea hapa,” alisema.

NGOZI HATARINI KUPOTEZA UBORA

Majaliwa alisema pamoja na uzalishaji wa ngozi nyingi nchini, lakini bidhaa hiyo iko hatarini kupoteza ubora kwa sababu watu wamekuwa wakichora mifugo.

“Tuache tabia ya kuandika majina au kuweka aina yoyote ya alama kwenye ngozi za wanyama, maeneo ambayo tumeruhusu alama zichorwe ni masikioni tu.

“Maofisa mifugo wote nchini waelimisheni wananchi kuacha kuandika na kuchora katika mifugo yetu. Hivi karibuni tunatarajiwa kumpokea mwekezaji kutoka Misri atakayewekeza kwenye ngozi,” alisema.

Pia aliwataka timu ya mawaziri nane iliyoteuliwa kuzunguka nchi nzima kutathmini migogoro ya wafugaji, kukamilisha mapema ripoti hiyo ili wananchi wajue hatma yao.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema maendeleo ya sekta ya kilimo na tasnia ya ushirika nchini, itaimarika baada ya kuzinduliwa mfumo rasmi wa mauzo ya mazao ya kilimo kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX). 

Alisema TMX, imeanzishwa kwa lengo la kuongeza ufanisi katika juhudi za Serikali za kurasimisha mifumo ya masoko ambayo imekuwa na changamoto kwa muda mrefu.

“Kwa kuwaunganisha wauzaji na wanunuzi wa bidhaa, kuleta ushindani kwenye bei, kupunguza gharama za uendeshaji biashara na kuweka uwazi,” alisema. 

Pia alisema kuzinduliwa kwa mfumo wa kielektoniki wa kusimamia biashara (ATMIS), utaimarisha makusanyo ya maduhuli na tozo kwa kuhakikisha huduma zote za utoaji vibali, leseni na vyeti unafanyika kielektroniki.

“Faida nyingine ni kuhakikisha kuwa kazi ya kumhudumia mteja inafanyika kwa wakati mara tu baada ya hatua zote za maombi ya utoaji vibali na vyeti kumalizika.  

“Pia kuimarisha upatikaji wa taarifa na takwimu muhimu za uingizaji na usafirishaji mazao ya kilimo nje ya nchi na kuondoa tatizo la nyaraka bandia ambalo huchangiwa na matumizi ya mfumo,” alisema Hasunga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,259FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles