Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk.Ashatu Kijaji amesema wana sababu ya kuwalinda wawekezaji wenye viwanda nchini kutokana na kutoa ajira kwa wananchi.
Dk. Ashatu amebainisha hayo leo Desemba 21,2023 jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea kiwanda cha Chemicotex kilichopo Mbezi Beach Jogoo kwa lengo la kuona bidhaa wanazozalisha na kuongea na wafanyakazi.
Amewaomba vijana wa kitanzania kuwa waadilifu na kujituma wanapopata ajira kwa kuweka kipaombele kwenye kufanya kazi ambazo wameaminiwa ili waendelee kunufaika kwa pamoja na kuimarisha uchumi wao na Taifa.
“Nimpongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa sababu ametengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na ufanyaji biashara,tunaona wawekezaji wanafuraha na amani wamekuja kuwekeza na wanaendelea kuzalisha,”amesema Dk. Ashatu.
Amesema kiwanda hicho cha mzawa kimeajiri watanzania 1000wanafanyakazi kiwandani na zaidi ya 1000 wanauza nje bidhaa.
Amesema kwa sababu kila unapokwenda unakutana na bidhaa za kiwanda hicho,ni muhimu kutambua kuwa wanatengeneza ajira kwa vijana na wanapata faida hivyo mitaji yao ipo salama.
Ameeleza kuwa kilichompa faraja zaidi asilimia 60 ya wafanyakazi 1000 ni wanawake.
“Sisi tupo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mmesikia bidhaa inayotengeneza hapa inauzwa kwenye nchi sita ndani ya Afrika na duniani tunapeleka bidhaa zetu,”ameongeza.
Aidha amesema wanaendelea kuimarisha Tanzania ya viwanda wanapotekeleza katika Dira ya Taifa wanakwenda kuhitimisha mwaka 2025 na kusisitiza viwanda ndio sehemu pekee watanzania wengi wanapata ajira.
Amesema wanavyojua dunia ipo kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda, hata dira inayoandaliwa sasa itawapa nafasi kubwa wenye viwanda.
Aidha ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda kuendelea kufurahia mazingira bora ya ufanyaji biashara.
Naye Mwenyekiti wa Kiwanda cha Chemicotex, Yogesh Manek amesema leo wamepata bahati ya kutembelewa na Waziri na kuona bidhaa wanazozalisha.
Amesema katika kiwanda hicho wanazalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo dawa za meno vipodozi na zinginezo.
“Asilimia kubwa ya watanzania wanatumia bidhaa ya kiwanda hiki tumeajiri jumla ya watu 1000 kati ya hao 550 wanawake na 450 wanaume na walemavu sita hii ni fursa kwa mtu yeyote anayetaka kufanya kazi,”amesema Manek.
Aidha amesema hali ya biashara kwa sasa ni nzuri kwa sababu wana fursa ya kufanya kazi na wanapeleka bidhaa zao nchi sita ikiwemo Rwanda, Unganda Uganda, Kenya, Burundi na Congo pamoja na soko la Tanzania.