31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Ashatu: Fanyeni utafiti kujua kinachoua biashara za wanawake

Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

MWAMKO wa biashara kwa wanawake umekuwa ukiongezeka siku hadi siku kutokana na hamasa na mazingira mazuri ya kufanyia biashara.

Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha mwaka 2014 Watanzania milioni 2.1 walikuwa wameajiriwa katika sekta rasmi ikiwa ni pamoja na serikalini na sekta binafsi.

Kulingana na takwimu hizo zaidi ya asilimia 60 ya wanawake walio kati ya umri wa miaka 18 hadi 24 yaani milioni 13.9 wanajishughulisha na shughuli zisizo rasmi biashara ndogondogo na kilimo. 

Shughuli hizo ni pamoja na kubuni bidhaa mbalimbali huku wengine wakifanya biashara katika vikundi au mtu mmoja mmoja.

Hata hivyo pamoja na jitihada hizi zinazofanywa na wanawake bado biashara zao nyingi hushindwa kuendelea na hufa mapema.

Hivi karibuni akizungumza katika mdahalo wa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kuhusu sekta ya fedha, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, aliagiza kufanywa utafiti kujua kinachosababisha asilimia 51 ya biashara zinazoanzishwa na wanawake nchini kufa kabla ya kufikisha miaka mitatu.

Dk. Ashatu anaiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kushirikiana na Mfuko wa Udhamini wa Sekta ya Fedha (FSDT) kutafuta sababu hizo.

Anasema pia watafute kinachosababisha wanawake kushindwa kurejesha mikopo inayotolewa na halmashauri.

Anasema kwa sasa mikopo inayotolewa na halmashauri ni chini ya asilimia 10 ndio inayorejeshwa. 

 “Niwaagize BoT na FSDT mwende vijijini na kufanya midahalo kama hii ili mje na majibu ya kwa nini asilimia 51 ya biashara za wanawake zinakufa kabla ya kusherehekea siku ya kuanzishwa ikitimiza miaka mitatu.

“Kwa nini mikopo inayotolewa na halmashauri kwa wanawake ni chini ya asilimia 10 tu ndio inarejeshwa?” anahoji Dk. Ashatu.

Anawataka waende wakazungumze na wanachi vijijini kujua sababu ya wao kutunza fedha katika vibubu badala ya kutumia taasisi za kifedha.

“Tunataka uchumi wa viwanda uliofungamanishwa na uchumi wa Watanzania wote lakini je, Watanzania wanajua wajibu wao kuelekea uchumi huu?” anahoji.

Naibu Waziri huyo anasema Serikali imeshusha gharama za watu kupata mitaji lakini cha kushangaza bado taasisi za fedha zimeshindwa kupunguza riba.

“BoT kaeni na taasisi za fedha wajibu hoja kwa nini bado hawajaanza kutekeleza agizo hilo mpaka sasa riba ziko juu,” anasema. 

Anaongeza kuwa waende kuwaeleza umuhimu na faida za wafanyabiashara wa Tanzania kurasimisha biashara zao. 

“Watanzania wengi hawataki kurasimisha biashara zao wanazofanya hivyo, ni jukumu lenu wasomi kuwaeleza umuhimu wa kufanya hivyo,” anasema Dk. Ashatu.   

Dk. Ashatu anasema hoja zilizoibuliwa na vijana katika mdahalo huo zinatakiwa kujadiliwa na vijana na wanawake wa vijijini, mitaani na shuleni ili elimu ya fedha iwafikie wengi zaidi.

“Niwaambie vijana kuwa mshindani wako pekee ni wewe ulivyokuwa jana hivyo, ni lazima tubadilike na kutumia changamoto hizi kama fursa za kujiongezea vipato,” anasema.

Kauli hiyo ya Naibu Waziri Ashatu kuhusu biashara za wanawake inaungwa mkono na mdau wa biashara kwa wanawake ambaye pia Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya K-Finance, Judith Minzi.

Akizungumza wakati wa maonyesho ya biashara ya wanawake yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, anasema biashara nyingi zinazoanzishwa na wanawake zimeshindwa kuendelea kwa sababu ya kukosa elimu ya biashara kwa wafanyabiashara hivyo kushindwa kujiendesha. 

“Ni muhimu kwa wafanyabiashara kutafuta elimu ya biashara kupitia njia mbalimbali ikiwamo mafunzo yanayotolewa na taasisi kadhaa hapa nchini,” anasema Judith.

Anasema wanawake wengi hawana elimu ya utunzaji wa fedha ikiwamo mikopo wanayokopa na kubaki na madeni makubwa.

Anasema wengi wao wanashindwa kutunza taarifa za biashara ambazo mara nyingi huhitajika katika hesabu za fedha kutokana na kukosa elimu.

Anaishauri Serikali kuanzisha somo la ujasiriamali kwa shule za msingi ili kuwajengea uwezo wanafunzi waweze kukua wakijua namna ya kufanya biashara.

Anasema sababu nyingine ni kutokujua namna ya kutafuta masoko na kwamba uelewa mdogo wa wafanyakazi wanaomsaidia mfanyabiashara kuuza bidhaa nalo ni changamoto ikiwa wengi watashindwa kujua vizuri biashara husika.

“Ni vyema wasaidizi wa mwanzilishi kujua maono aliyonayo na wazo la biashara lilivyo wakati wanasaidia kutafuta masoko,” anasema Judith.

Anasema sababu nyingine ni wanawake wengi kunakili biashara ambayo anafanya mtu bila kujua wazo lake namna lilivyoanzishwa.

Anasema wanawake wengi wanapoanzisha biashara hawawi wabunifu bali wao hukurupuka baada ya kuona biashara za wengine.

 “Kumekuwa na tabia kuangalia biashara ya mtu aliyefanikiwa bila kujua namna gani aliona fursa katika biashara hiyo, na mwingine anaingia bila kuifanyia utafiti wa kina,” anasema Judith.

Judith anasema upatikanaji wa mtaji wa biashara pia umekuwa ni mzigo kwa wanawake kutokana na kuwa na riba kubwa.

“Sababu nyingine ni upatikanaji wa mitaji kama ni nafuu au ni mkopo wenye gharama kubwa kiasi ambacho mfanyabiashara anajikuta akiutumikia mtaji muda wote kwa kulipa deni,” anasema.

Anasema pia uoga kwa wanafunzi kusoma somo la hesabu wanapokuwa shuleni hivyo wanapokuwa wakubwa kushindwa kufanya vema katika biashara.

“Tuendelee kushawishi wanafunzi wapende kusoma hesabu kwani inasaidia katika uanzishaji na usimamizi wa biashara,” anasema Judith. 

Anasema kwa kuliona hilo taasisi ya K-Finance imeandaa mafunzo kwa wajasiriamali yatakayofanyika Januari 18, 2020 jijini Dar es Salaam kwa kufundisha jinsi ya kutumia vipaji kuufikia uhuru wa kiuchumi. 

Anasema katika uchunguzi walioufanya wamebaini kuwa watu wengi wanaoanzisha biashara wanashindwa kufikia malengo kutokana na kutokuwa na elimu hiyo.

Anasema mafunzo hayo yatasaidia kuwapa uelewa wa biashara wanazofanya na watakazoanzisha ili kuziwezesha kuwa imara na kudumu kwa muda mrefu.

“Tutawakutanisha wafanyabiashara waliofanikiwa na ambao wanaanza ili kubadilishana uzoefu na changamoto zinazopatikana katika ufanyaji biashara,” anasema Judith.

Anasema wafanyabiashara wengi waliofanikiwa wamepitia changamoto mbalimbali ambazo wakibadilishana na wanaoanzisha biashara zitawasaidia kujua namna ya kuzitatua watakapokumbana nazo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles