Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wahitimu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa ambao ni waumini wa dini ya Kiislamu wametakiwa kujiepusha na mmomonyoko wa maadili na kuishi katika misingi ya uislamu.
Wito huo umetolewa Oktoba 14,2023 na Diwani wa Viti Maalumu Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Asha Johari, wakati wa mahafali ya kidato cha nne kwa wanafunzi wa Kiislamu katika shule hiyo.
Amesema vijana wanatakiwa kutambua mema na mabaya na kuishi katika misingi ya uislamu.
“Mmemaliza kidato cha nne ndio mnaanza msingi wa kwenda juu, jiepusheni na vitendo viovu mtashindwa kutimiza ndoto zenu. Sisi ni waislamu tuishi katika maisha ya uislamu,” amesema Johari.
Diwani huyo pia amewataka wanafunzi huo kujiamini wakati wa mtihani huku wakimtanguliza Mungu wakati wote.
Kiongozi wa Jumuiya ya Wanafunzi Waislamu Benjamin Mkapa, Muktari Ayubu, amesema ilianzishwa mwaka 2000 na mpaka sasa inasimamia wanafunzi 700 wakiwemo wasichana 390 na wavulana 310.
Amesema wamefanikiwa kupata sehemu ya kuswalia ndani ya shule, kutoa elimu ya dini na kuwasaidia wanafunzi 20 wanaoishi kwenye mazingira magumu.
“Tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kutusaidia vitabu vya dini, kuwalipa walimu wanaojitolea kuja kutufundisha na kuwasaidia wanafunzi wenzetu wasiojiweza kwa kuwapatia sare za shule, nauli na fedha za kujikimu kwa sababu tumekuwa tukichangishana kila siku ili kuwasaidia,” amesema Ayubu.