Na RAYMOND MINJA – IRINGA
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Mafinga mkoani Iringa, jana limemsimamisha Diwani wa Kata ya Boma, Julist Kisoma (Chadema) kutokuhudhuria vikao vya baraza hilo kwa tuhuma za kuidanganya Tume ya Uchaguzi na wananchi wake kuwa anajua kusoma na kuandika.
Kugundulika kwa diwani huyo kutokujua kusoma na kuandika, kulikuja baada ya kukacha kusoma taarifa ya kata yake mara tatu mfululizo, hali iliyoilazimu kamati ya maadili ya baraza hilo kufanyia kazi tuhuma zilizokuwa zikimkabili za kuidanganya Tume ya Taifa ya Uchanguzi kuwa anajua kusoma na kuandika wakati si kweli.
Taarifa zilizoifikia MTANZANIA Jumapili na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Charles Makoga, zilisema kuwa diwani huyo amesimamishwa kutokuhudhuria vikao na shughuli zozote za kuwawakilisha wananchi hadi pale tume itakapotoa uamuzi juu yake.
Makogo alisema awali walisikia taarifa za diwani huyo kutokujua kusoma na kuandika, lakini walikuwa hawana uhakika nazo hadi walipokuja kupata shaka baada ya kukimbia mara tatu kusoma taarifa za kata yake.
“Unajua katika baraza letu tuna utaratibu wa kila robo mwaka madiwani huwa wanasoma taarifa ya kata zao, sasa mara ya kwanza aliomba udhuru akisema macho yake yanamsumbua, hivyo hawezi kusoma vizuri,” alisema.
Makoga alisema kuwa mara baada ya kupeleka tuhuma hizo kamati ya maadili ambayo ilimuita mhusika kumuhoji, alikiri kuwa hana uwezo wa kusoma mbali kwa kuwa ana matatizo ya macho na tayari daktari wake alishamwambia kuwa hatakuwa na uwezo kusoma vizuri.
Alisema kuwa mara baada ya tume hiyo kujiridhisha na kumaliza uchunguzi wao, aliombwa na kamati hiyo kuitisha kikao cha madiwani cha dharura kwa mujibu wa kanuni za baraza hilo ili kuweza kujadili jambo hilo na ndipo walipofikia uamuzi wa kumsimamisha diwani huyo.
Makoga alisema kuwa ni kosa kisheria kwa mtu kudanganya kuhusu kiwango cha elimu aliyonayo, hasa akiwa kiongozi.