DIWANI CCM MBARONI KWA RUSHWA YA 500,000/-

0
529

Vector illustration of a man lock up in prison

Na MOHAMED HAMAD,KITETO

DIWANI wa Kata ya Ndirigishi mkoani Manyara, Chitu Daima (CCM), anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za kudai na kupokea rushwa ya Sh 500,000.

Tukio hilo limetokea kijijini hapo baada ya wananchi kumtuhumu Chitu kupokea rushwa ndipo wakaamua kutega mtego na kufanikiwa kumnasa akipokea kutoka kwa mmoja wao.

Kwa mujibu wa Ainoti Sepewa mmoja wa wafugaji aliyedaiwa fedha hiyo ili aweze kupatiwa maeneo ya kulisha mifugo yao, alisema awali walimpa zaidi ya Sh milioni moja bila mafanikio ya kupata maeneo kwa ajili ya shughuli za ufugaji.

“Baada ya kuchoshwa na hali hii, nililazimika kwenda PCCB kuomba msaada zaidi, ndipo akataka nimpe laki tano nikamwahidi kuwa naenda mnadani kuuza ng’ombe na kufanikiwa kupewa fedha na PCCB na kumkamatisha,” alisema Sepewa.

Alisema awali wananchi kwa pamoja walikubaliana kumega sehemu ya Hifadhi ya Emboley Murtangos ili wagawane wakulima na wafugaji, badala yake eneo hilo limegawiwa wakulima peke yao na kusababisha manung’uniko makubwa.

Kwa upande wake mwananchi mwingine, Mathew Isaya, alitaja baadhi ya madhara waliyopata kutokana na rushwa hizo kuwa ni pamoja na kutopatikana haki na kusababisha uhusiano mbaya kati ya wakulima na wafugaji kupigana.

Naye Kadege Mario wa Kitongoji cha Kuti, Kijiji cha Ndirigishi, alisema mara ya kwanza walimpa Sh 500,000, Sh 300,000 na siku nyingine walimpa Sh 400,000 na mbuzi mmoja akisema maisha yao ni duni.

Kwa upande wake, Kamanda wa Takukuru Wilaya ya Kiteto, Jastine Maingu, amekiri kutokea kwa tukio hilo akisema hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa wako katika hatua ya awali pamoja na kufanya mahojiano juu ya tukio hilo na hadi sasa mtuhumiwa anashikiliwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here