23.7 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

Diwani aandaa mafunzo ya kujitambua kwa vikundi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wanavikundi 74 kutoka Kata ya Bonyokwa wamepatiwa mafunzo ya kujitambua ili wajue wajibu wao katika uendeshaji wa vikundi hivyo.

Mafunzo hayo ambayo pia yamehudhuriwa na wenyeviti wa mitaa, ofisa maendeleo na viongozi wa dini yaliandaliwa na Diwani wa Kata ya Bonyokwa, Tumike Malilo, huku Mkufunzi akiwa ni Mkurugenzi Sauti ya Jamii Kipunguni, Selemani Bishagazi.

Baadhi ya wanavikundi kutoka Kata ya Bonyokwa wakiwa kwenye majadiliano wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Diwani wa kata hiyo, Tumike Malilo (hayupo pichani).

Tumike amesema ameamua kuanza na mafunzo ya kujitambua ili vikundi vijue wajibu wake na kujitathmini.

“Naamini kuanzia kwa viongozi na wanachama kila mmoja akitambua wajibu wake na akautimiza tutasonga mbele, kwa sasa usishangae kukuta mwenyekiti anafanya kazi za mhasibu, au kukuta vikundi vingine watu wawili wanapitisha maamuzi badala ya mkutano mkuu wa kikundi.

“Pia tunataka tutumie fursa ya vikundi kuzuia ukatili kwa wanawake, watoto na wasichana,” amesema Tumike.

Amesema pia anataka kuona vikundi vinakuwa na uelewa sio tu wa ujasiriamali bali hata masuala ya haki na nidhamu katika matumizi ya fedha.

“Wanawake na vijana wengi wamekuwa wakifanya biashara lakini fedha zao zinaishia wapi ndio mtihani, kupitia mafunzo haya tunataka kufungua ukurasa mpya,” amesema.

Kwa mujibu wa Tumike mafunzo hayo yatakuwa endelevu kwa muda wa miezi mitatu ambapo yatatolewa mara mbili kwa mwezi ili kuiwezesha kata hiyo iwe ya mfano na ikiwezekana mwakani kwa wilaya ya Ilala kikundi bora kitoke Bonyokwa.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake Leokadia Stefano, amesema amejifunza vitu vipya ambavyo awali hakufahamu kama kikundi kinaweza kutumika kuzuia ukatili wa kijinsia.

“Mimi nlikuwa naamini kwamba jukumu la kuzuia ukatili ni la viongozi na polisi lakini kuanzia sasa nimefunguka, tumekuwa tukiendesha vikundi kienyeji ila kwa mafunzo haya tunaenda kubadilika,” amesema Leokadia.

Mafunzo yaliyotolewa ni nidhamu katika matumizi, uwajibikaji, muundo wa uongozi wa vikundi, umuhimu wa kutunza kumbukumbu, namna ya kuibua na kuandaa miradi ya vikundi, fursa zinazopatikana kwenye mashirika mbalimbali yanayofanya kazi na vikundi na namna ya kuripoti vitendo vya ukatili ikiwemo rushwa ya ngono.

Akiahirisha mafunzo hayo Ofisa Maendeleo wa Kata ya Bonyokwa, Regina Ng’ongolo, amemshukuru diwani huyo kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatasaidia vikundi kutimiza wajibu wake ipasavyo.

“Namshukuru mheshimiwa diwani kwa kuona umuhimu wa kuleta mafunzo haya ambayo yamekuja wakati muafaka, kumekuwa na tatizo la baadhi ya vikundi kutotimiza wajibu wake ambapo inatupa shida sisi maofisa maendeleo naamini huu utakuwa muarobaini. Nitashirikiana na mheshimiwa diwani kuhakikisha vikundi vyote vinapigwa msasa ili kata yetu iwe ya mfano,” amesema Regina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,745FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles