27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

DIT YAZINDUA MAFUNZO KWA MAFUNDI SIMU ZA MKONONI

NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

CHUO cha Teknolojia Dara es Salaam (DIT), kimezindua mafunzo ya muda mfupi kwa mafundi simu baada ya kubaini wengi wao hawana elimu ya kutosha kufanya kazi hiyo.

Mafunzo hayo yalizinduliwa jana baada ya kufanya utafiti kwa mafundi 261 wa Dar es Salaam na Morogoro na kubaini upungufu uliopo ndipo ikaonekana ni vyema ukatengenezwa mtaala wa mafunzo hayo.

Akizungumzia kozi hiyo ambayo tayari ina wanafunzi 109, Mratibu wa Mafunzo hayo, Dk. Petro Pesha, alisema utafiti uliangalia kiwango cha ujuzi walichokuwa nacho mafundi hao, uelewa na mazingira ya kazi wanayofanyia.

“Mafundi 170 walitoka Dar es Salaam na mafundi 91 walioshiriki katika utafiti walitoka Morogoro, utafiti unaonesha asilimia 54 walipata mafunzo, asilimia 80 walipata mafunzo katika mfumo usio rasmi, asilimia 67 hawajui sheria na utaratibu na asilimia 80 hawana elimu ya ujasiriamali,” alisema Dk. Pesha.

Alisema madhumuni ya kutoa mafunzo hayo ni kuwawezesha mafundi hao kuzingatia sheria, kutumia vifaa kwa usahihi na kuwaonyesha njia sahihi ya ujasiriamali.

Pia alisema mafunzo hayo yatakuwa kwa awamu tatu, awamu ya kwanza mwezi mmoja, ya pili mwezi mmoja na nusu na awamu ya tatu wiki mbili.

Kwa upande wake, Mkuu wa DIT, Profesa Preksedis Ndomba, alisema wanaandaa rasilimali watu watakaowezesha nchi kufikia katika uchumi wa viwanda.

Alisema wananchi waendelee kuhamasishana mafundi simu wote wapate mafunzo kisha wapewe leseni na vifaa zaidi vipatikane kwa ajili ya kuboresha kozi hiyo.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Conie Francis, alisema matumizi ya simu yameongezeka kwa kiwango kikubwa na kwa sasa kuna laini milioni 43 za simu.

Alisema wanafunzi hao watafundishwa kanuni mbalimbali ikiwemo kanuni ya kumlinda mtumiaji wa simu.

Naye Kamishna wa Polisi anayeshughulikia Uhalifu wa Mtandao, Shaabani Mhiki, alisema vimejitokeza vitendo vya uvunjifu wa amani kupitia simu za mkononi hivyo kozi hiyo fupi itasaidia kupunguza uhalifu huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles