Director Kenny: Fundi umeme anayepeta katikati ya Harmonize, Mondi

0
1463

Christopher Msekena

SAFARI za mastaa wa Bongo Fleva kupanda ndege kwenda Afrika Kusini na kwingineko duniani kwaajili ya kufanya video zimekoma ndani ya miaka ya hivi karibuni, mara baada ya kuibuka kwa waongozaji mahiri wenye uwezo wa kuzalisha video zenye ubora mkubwa.

Miongoni mwa waongozaji waliofanikiwa kuiteka tasnia hiyo kwa kuzalisha video kubwa zilizoleta mapinduzi ndani na nje ya Tanzania ni Director Kenny, mwongozaji wa video kutoka kampuni ya Zoom Production inayomilikiwa na Diamond Platnumz na Harmonize.

Swaggaz, tumefanya mahojiano yafuatayo  na Director Kenny ambaye amefanikiwa kuongoza video nyingi za wasanii wa WCB  na nje ya lebo hiyo ikiwamo  Yo Pe  Remix ya Innoss B na Diamond Platnumz inayoshika namba moja sasa kwa kutazamwa kwenye mtandao wa YouTube.

SWAGGAZ: Kenny ni nani na uliingia vipi kwenye tasnia hii ya uongozaji wa video?

Kenny: Nimezaliwa jijini Mbeya miaka kadhaa iliyopita nikasoma shule ya Kambarage baada ya hapo nikajiunga na chuo kusomea masuala ya umeme. Nilipomaliza nikawa napenda mambo ya video nikaja Dar es Salaam kusoma online kuhusu video kama miezi sita hivi.

Baada ya hapo nikaanza kutafuta ‘connection’ na kama unavyojua ukishamaliza masomo lazima ufanye ‘field’ (mafunzo kwa vitendo), nikakutana na Hanscana tukatambulishana na video ya Darassa na Rich Mavoko inaitwa Kama Utanipenda ndiyo video yangu ya kwanza kushuudia ikifanywa.

Kuanzia hapo nikaanza kujua, kupangilia rangi na kuhariri video na wakati huo nikawa nakutana na wasanii wengi. Harmonize ni miongoni mwa wasanii ambao tulikuwa tukikutana tunapiga stori nyingi sana, akaniambia kwanini nisiwe nafanya video zangu mwenyewe, tukakaa chini tukapanga vitu, akanitambulisha Wasafi nikaonana na Lava Lava  ambaye nilifanya naye video yangu ya kwanza inaitwa Dede.

Baada ya kufanya Dede, video ikapelekwa WCB kila mtu akaikubali, kuanzia hapo ukaribu wangu na WCB ukaanza nikawa nafanya video za wasanii wote ambao watakubaliana na mimi.

SWAGGAZ: Kabla hujafanya video mambo gani muhimu ambayo huwa unazingatia na msanii anapaswa kuwa na vigezo gani?

Kenny: Kwanza lazima ujue ratiba, muda, ninayefanya naye kazi, wimbo wenyewe upo vipi hayo ndiyo mambo muhimu ninayozingatia. Kwa msanii awe vyovyote kiasi cha kuweza kunimudu mimi na bajeti yangu sababu mimi nafanya biashara.

SWAGGAZ: Umeongoza video za wasanii wengi, msanii gani ni msumbufu kwamaana ya kujenga mnapokuwa ‘location’?

Kenny: Karibia wasanii wote ninaofanya nao kazi wana hiyo tabia na mimi huwa nasikiliza pia mawazo yao sababu lengo ni kutoa video kali.

SWAGGAZ: Changamoto zipi unakutana nazo katika kazi zako?

Kenny: Changamoto kubwa ambayo nakumbana nayo ni ni muda, nipo bize sana na nyingine za kawaida.

SWAGGAZ: Mpaka sasa umefanikiwa kupata mafanikio gani?

Kenny: Mafanikio yapo mengi, siwezi kuyataja yote ila yapo.

SWAGGAZ: Tunafahamu Harmonize ni miongoni mwa wawekezaji pale Zoom Production, je kuondoka kwake WCB kumeathiri chochote kwenye kazi zako?

Kenny: Hamna hainiathiri chochote kwa ufupi mimi nipo katikati, siangalii huku au kule vipi, mimi nasubiri nipewe nyimbo nifanye video shughuli iishe, wenyewe huko watajuana lakini kazi yangu mimi ni hiyo.

SWAGGAZ: Umefanikiwa kuingia kwenye tuzo nchini Marekani, je ni tuzo gani na mashabiki wanaweza vipi kukupigia kura?

Kenny: Kwanza nimejisikia vizuri sana kuwa mwongozaji wa kwanza kuingia kwenye tuzo za Afrimma za Marekani na zile za Nigeria, kwangu ni jambo kubwa na watu wanaweza kunipigia kura kwa kuingia kwenye ukurasa wangu wa Instagram @director_kenny, pale kwenye bio wakigusa link itawapeleka moja kwa moja kwenye kipingele cha Best Video Director (Mwongozaji Bora wa Video) na zile Afrima za Nigeria watu waende kwenye bio ya Instagram @zoom_production wakigusa link itawapeleka moja kwa moja kunipigia kura kama Mwongozaji Bora wa Video ya Kiafrika.

SWAGGAZ: Video gani imekupa mafanikio zaidi toka uanze kufanya kazi hiyo?

Kenny: Video nyingi zimenipa mafanikio, kila video inaleta mafanikio yake, kuna video inaweza kukupa fedha, kuna nyingine zinaweza kukupa kujulikana na nyingine zinaweza kukupa dili.

SWAGGAZ: Asante kwa muda wako.

Kenny: Shukrani sana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here